ULEGA AWEKA NDANI WAKANDARASI WAZEMBE. - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Friday, November 21, 2025

ULEGA AWEKA NDANI WAKANDARASI WAZEMBE.

 


Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega ameagiza kuwekwa ndani kwa wakandarasi wa kampuni kutoka China ambao wameshindwa kutimiza masharti ya mkataba wa ujenzi wa barabara ingawa serikali imetimiwa wajibu wake kwa kulipa sehemu ya malipo.


Ulega amesema juhudi za kutaka vigogo wa kampuni hiyo kuja nchini na kutoa maelezo kuhusu kusuasua kwa ujenzi wa barabara waliyopewa kujenga mkoani Dodoma, zimegonga mwamba hadi sasa na sasa kuna uwezekano wa kuwafikisha mahakamani kwa kukiuka masharti ya mkataba.


Kampuni hiyo China First Highway Engineering Co. Ltd.imepewa kazi ya ujenzi wa Sehemu ya pili ya barabara ya Ntyuka- Mvumi Hospitali- Kikombo (Km 53) na ingawa tayari imepewa asilimia kumi ya malipo (kiasi cha shilingi bilioni 9.68) ujenzi umefikia asilimia mbili tu.


“Kuanzia sasa hivi, mkandarasi mzembe, mwenye dharau na asiyeendana na ratiba ya mkataba hatutamvumilia na hatua kali za kimkataba zitachukuliwa dhidi yake. Sisi tutaendelea kufanya kazi na kuenzi wakandarasi wanaotimiza majukumu yao lakini wale ambao wamepokea fedha zetu lakini hawatimizi upande wao wa mkataba hao tutachukua hatua. Kazi iendelee,” alisema. 


Waziri huyo ameagiza Jeshi la Polisi na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) kumshikilia na kumuhoji mkandarasi huyo ambaye alipaswa kufikisha asilimia 13 ya utekelezaji wa mradi huo kufikia sasa hivyo kushindwa kuendana na kasi ya ujenzi licha ya kulipwa fedha kwa wakati.

Aidha, Ulega amesema kuwa licha ya hatua hiyo aliyoichukua pia ataifuatilia miradi mingine inayotekelezwa na mkandarasi huyo na kuahidi kuichukulia hatua zaidi endapo hatoridhishwa na hivyo amemuagiza Naibu Katibu Mkuu, Dkt. Charles Msonde kuifuatilia kama inaendelea kwa mujibu wa mkataba. 


Waziri huyo ambaye pia Mbunge wa Jimbo la Mkuranga amewataka watendaji wote wa Wizara ya Ujenzi kuhakikisha miradi yote inayojengwa inapewa wakandarasi wenye uwezo na wenye uzoefu wa kumaliza miradi kwa wakati.


Amemtaka Mkandarasi CHICO anayejenga sehemu ya Ntyuka- Mvumi- Makulu (Km 8.6) na Kikombo- Chololo – Mapinduzi (Km16.4) kuongeza kasi ya ujenzi wa madaraja kabla ya kipindi cha mvua zinazotarajiwa kuanza hivi karibuni.


Katika hatua nyingine amemtaka Mkandarasi BCEG anayetekeleza mradi wa jengo la abiria katika Kiwanja cha ndege cha Msalato kuhakikisha anaongeza kasi ya ujenzi kwa kuwa Serikali haitamuongezea muda na kumtaka akamilishe ujenzi huo kwa mujibu wa mkataba.


Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu, Dkt. Charles Msonde amemhakikishia Waziri wa Ujenzi kuwa watayafanyia kazi maelekezo hayo haraka iwezekanavyo ili kupatia ufumbuzi changamoto za miradi yote inayosuasua.

 

Naye, Meneja wa TANROADS Mkoa wa Dodoma, Mhandisi, Zuhura Amani amesema kuwa wataendelea kuwafuatilia na kuwasisitiza makandarasi wote wanaotekeleza miradi hiyo kuhakikisha wanaendelea kufanya kazi kwa mujibu wa mkataba.


Ujenzi wa Barabara ya Ntyuka- Mvumi- Makutano ya Kikombo (Km 76) umegawanyika katika Awamu mbili za Ntyuka- Mvumi- Makulu (Km 8.6) na Kikombo- Chololo – Mapinduzi (Km16.4) pamoja na Sehemu ya Pili ya barabara hiyo ya Ntyuka- Mvumi Hospitali- Kikombo (Km 53) ambapo sehemu zote zinagharamiwa na Serikali kwa asilimia miamoja ikiwa ni mkakati wa Serikali wa kuunganisha jiji la Dodoma na vitongoji vyake kwa Barabara za lami na hivyo kupunguza msongamano na kuchochea Uchumi.













No comments:

Post a Comment