WALENGWA WA MRADI WA PAMOJA WATAFUTIWE MASOKO - DKT. MUSSA - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Saturday, November 15, 2025

WALENGWA WA MRADI WA PAMOJA WATAFUTIWE MASOKO - DKT. MUSSA


Katibu Tawala Mkoa wa Morogoro Dkt. Mussa Ali Mussa amewataka waratibu na watalaam kutoka katika Halmashauri zinazotekeleza Mradi wa Kukuza Usawa wa Kijinsia Tanzania Bara (PAMOJA) kuhakikisha wanakwenda kutafuta masoko ya bidhaa za walengwa wa mradi huo ili kuwawezesha kupata kipato kitakachoinua uchumi wao.

Dkt. Mussa ametoa wito huo mjini Morogogoro katika Ukumbi wa Chuo Kikuu cha Jordan, wakati akifunga mafunzo ya kuzijengea uelewa timu za utekelezaji wa mradi ili ziweze kutekeleza kikamilifu jukumu la kuimarisha fursa za kiuchumi kwa wanawake wa vijijini, kuzuia ukatili pamoja na kutoa huduma kwa manusura wa vitendo vya ukatili wa kijinsia.

“Kama ni kweli mmedhamiria kuwawezesha walengwa wa mradi wa PAMOJA kupiga hatua kimaendeleo, ni lazima kuwatafutia masoko ya bidhaa zao wanazozizalisha,” Dkt. Mussa amesisitiza.

Dkt. Mussa ameongeza kuwa, waratibu na watalaam hao wa mradi wa PAMOJA wanapaswa kuziongezea thamani shughuli za walengwa wa mradi na kuhakikisha wanafanya kazi kwa ushirikiano, ili kupanua wigo wa ajira kwa walengwa wengine pamoja na kuleta matokeo chanya kama ilivyokusudiwa na Serikali.

Mmoja wa waratibu wa mradi wa PAMOJA, ambaye ni Afisa Maendeleo Mkoa wa Geita Bi. Marth Kaloso ameahidi kuwa watahakikisha utekelezaji wa mradi unazingatia thamani ya fedha iliyotolewa, watatoa elimu ya ukuzaji wa miradi pamoja na kuhakikisha kuna ulinzi na usalama kwa watoto.

Kwa upande wake, Bw. Wanchoke Chichibela ambaye ni Mratibu wa Mradi wa Pamoja Mkoa wa Mara amesema kuwa wataenda kutoa elimu ya ujasiriamali, elimu ya kuweka akiba na kukopa ili mikopo itakayotolewa kupitia Mradi wa Pamoja iwawezeshe akina mama kujikomboa kiuchumi.


Kwa upande wake, Meneja Mahusiano Dhamana za Wateja kutoka Benki ya NMB Bi. Monica George amesema watawezesha ufunguaji wa akaunti ya mradi, ufunguaji wa akaunti za walengwa wa mradi, kutoa elimu ya fedha na mikopo ili walengwa waweze kufanya shughuli walizokusudia pamoja na kufanya marejesho kwa wakati ili fedha za mradi wa PAMOJA ziwasaidie pia walengwa wengine.


Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais-TAMISEMI zimeweza kutoa mafunzo kwa waratibu na wataalam kutoka katika halmashauri 40 zinazonufaika na Mradi wa PAMOJA, waratibu na wataalam hao wanatoka katika Mikoa 10 ya Tanzania Bara ambayo ni Mwanza, Kagera, Mara, Shinyanga, Simiyu, Geita, Singida, Tabora, Rukwa na Arusha.




No comments:

Post a Comment