
Na Mwandishi, Mbeya
Mwakilishi wa Katibu Tawala wa Mkoa wa Mbeya, Simon Parmet ameipongeza Wizara ya Nishati kwa kutoa elimu kwa Maafisa Dawati kuhusu matumizi ya nishati safi ya kupikia, hatua ambayo itachochea kasi ya utekelezaji wa Mkakati wa Kitaifa wa Nishati Safi ya Kupikia na kusaidia kufikia malengo ya Serikali ya kuwa na asilimia 80 ya watanzania wanaotumia nishati safi ifikapo mwaka 2034.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo ya maafisa wanaoratibu utekelezaji wa mkakati huo kwa Mikoa na Halmashauri za Nyanda za Juu, yaliyofanyika mkoani Mbeya leo Novemba 10, 2025, Parmet amesema elimu hiyo imekuja kwa wakati muafaka kwa kuwa mikoa hiyo inaongoza kwa kilimo na uzalishaji wa mazao ya miti, lakini bado matumizi ya kuni na mkaa ni makubwa
“Mikoa hii inaongoza kwa kilimo cha miti, lakini pia matumizi ya kuni ni makubwa. Elimu hii itasaidia Maafisa Dawati kuelimisha wananchi kuhusu umuhimu wa kutumia nishati safi ya kupikia na kuachana na mapishi ya mazoea,” alisema Parmet.
Kwa upande wake, Mwakilishi wa Mkurugenzi wa Nishati Safi ya Kupikia kutoka Wizara ya Nishati, Bw. Benezeth Kabunduguru amesema kuwa mafunzo hayo ni endelevu kwa kuwa yatatolewa katika madawati ya waratibu wa mikoa yote nchini ili kila mmoja apate uelewa zaidi wa nishati safi ya kupikia na kuweza kuwafikia wananchi kwa urahisi na wakati wote.
“Tunataka kila afisa dawati awe na uelewa wa kina kuhusu nishati safi ya kupikia ili aweze kuwafikia wananchi kwa ufanisi. Lengo letu ni kufikia asilimia 80 ya matumizi ya nishati safi ifikapo mwaka 2034,” alisisitiza Kabunduguru.
Amesisitiza kuwa kuwa suala la matumizi ya nishati safi ya kupikia ni kipaumbele cha nchi na dunia kwa ujumla ili kuondokana na athari zake katika mazingira, afya na kiuchumi, hivyo mafunzo hayo yanatolewa katika makundi mbalimbali katika mikoa yote 26 nchini.
Kwa upande wake, Afisa Mwandamizi mshauri masuala ya kiufundi kutoka Wakala wa Nishati Vijijini ( REA), Mhandisi Deusdedit Malulu aliwahimiza Maafisa Dawati kutumia mafunzo hayo kutangaza fursa zilizopo katika sekta ya nishati safi ya kupikia, ikiwemo ufadhili wa miradi, utengenezaji wa majiko banifu, uzalishaji wa mkaa mbadala, na uanzishaji wa vikundi vya ujasiriamali vitakavyoweza kunufaika na ruzuku za REA.
Ametaja baadhi ya fursa hizo kuwa ni pamoja na kutengeza majiko banifu, mkaa mbadala pamoja na kuanzisha vikundi vya ujasiriamali vitavyoweza kupewa ruzuku katika sekta hiyo.
Mafunzo hao yamehusisha maafisa dawati wa Halmashauri na Mikoa ya Mbeya, Iringa, Songwe, Katavi, Rukwa, Njombe na Ruvuma.




No comments:
Post a Comment