
Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. Asha-Rose Migiro, amewataka wanawake nchini kuwa mstari wa mbele katika kulinda na kuimarisha amani, akisisitiza kuwa matukio yaliyotokea Oktoba 2025 hayawakilishi utamaduni wa Tanzania.
Dk. Migiro alitoa ujumbe huo Desemba 4, 2025, wakati akifungua Jukwaa la Wanawake 2025 lililobeba kaulimbiu “Mama ni Amani”.
Hafla hiyo imefanyika katika Jijini Dodoma na kuhudhuriwa na wanawake kutoka mikoa mbalimbali pamoja na wageni kutoka Zanzibar.
Kabla ya ufunguzi, ilioneshwa makala ya video iliyodokeza matukio ya Oktoba 29, 2025, ikieleza thamani ya mali zilizoharibiwa na taarifa za vifo, ingawa idadi ya waliopoteza maisha haikutajwa.
Katika hotuba yake, Dk. Migiro amesema kuwa huu ni wakati muafaka wa kuanza mazungumzo ya kitaifa yatakayozalisha maridhiano na kuirejesha Tanzania katika hadhi yake kama nchi ya amani na utulivu. Amesisitiza kuwa wanawake wana nafasi muhimu katika kuongoza mchakato huo.
“Lengo ni kuhakikisha nchi inabaki salama. Huu siyo utamaduni wetu. Tujipange kwa ajili ya mazungumzo yatakayoleta maridhiano,” amesema Dk. Migiro.
Ameeleza kuwa zaidi ya asilimia 50 ya Watanzania ni vijana, hivyo wanawake wanapaswa kusimama imara kuhakikisha matukio ya vurugu hayajirudii, kwa kuongoza juhudi za uponyaji na malezi bora.
Mmoja wa washiriki, Kate Kamba, amesema mwanamke ndiye mlezi wa kwanza na mwalimu wa familia, hivyo hapaswi kukwepa wajibu wake katika kujenga misingi imara ya malezi ili kuepusha machafuko ya baadaye.
Ameonya kuwa bila kuwekeza katika malezi na misingi bora, taifa linaweza kupoteza mwelekeo, lakini wanawake wakisimama kwa umoja wao kupitia vijana, Tanzania itaendelea kuwa mfano wa kuigwa katika kudumisha amani.
Kwa upande wake, Sifa Swai, amesema changamoto za usalama wa amani zimehamia zaidi kwenye mitandao ya kijamii ambako taarifa potofu huzagaa kwa kasi, na kusababisha vijana kupoteza mwelekeo.
Ameongeza kuwa mtikisiko kwenye biashara za wanawake mara nyingi huathiri ustawi wa familia na hatimaye kusababisha machafuko ya kijamii.
Washiriki wa jukwaa hilo kwa pamoja wametilia mkazo umuhimu wa sauti ya mwanamke katika kulinda amani, kuponya makovu ya kijamii na kuongoza juhudi za maridhiano nchini.






No comments:
Post a Comment