WATUMISHI WA TUME YA MADINI WATAKIWA KUZINGATIA UWAJIBIKAJI NA UADILIFU - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Thursday, December 4, 2025

WATUMISHI WA TUME YA MADINI WATAKIWA KUZINGATIA UWAJIBIKAJI NA UADILIFU




Na Mwandishi Wetu, Dodoma


Watumishi wa Tume ya Madini wametakiwa kuimarisha uwajibikaji, uadilifu na uwazi, sambamba na kuongeza uelewa kuhusu athari za rushwa na mbinu za kuikabili katika utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku ili kuhakikisha huduma bora na matokeo yenye tija kwa taifa.

Wito huo umetolewa leo, Desemba 4, 2025, na Mkurugenzi wa Rasilimali Watu na Utawala wa Tume ya Madini, Nsajigwa Kabigi, akimwakilisha Katibu Mtendaji wa Tume Mhandisi Ramadhani Lwamo, wakati wa mafunzo ya maadili ya utumishi wa umma na masuala ya rushwa yaliyofanyika katika Ukumbi wa Tanzanite, Makao Makuu ya Tume ya Madini jijini Dodoma.


Akizungumza katika mafunzo hayo, Kabigi amesema sekta ya madini ina vishawishi vingi kutokana na majukumu yake ya ukusanyaji wa maduhuli na uhusiano wa karibu na wadau mbalimbali, hivyo kuhitaji watumishi wenye misimamo thabiti ya uadilifu na uzingatiaji wa maadili.

Amesisitiza kuwa mapambano dhidi ya rushwa ni wajibu wa kila mtumishi, akibainisha kwamba “kila mmoja wetu ni muathirika wa rushwa moja kwa moja au kupitia watu wanaotuzunguka, hivyo kupambana na rushwa ni jukumu letu sote.”

Ameongeza kuwa mafunzo hayo yamelenga kuwajengea watumishi uelewa mpana kuhusu maadili ya utumishi wa umma, haki na wajibu wa watumishi katika maeneo ya kazi, pamoja na kuimarisha utendaji bora unaoendana na miongozo ya serikali.

Kabigi amewataka washiriki wa mafunzo kusambaza elimu waliyoipata kwa watumishi wenzao ili kuboresha utoaji huduma na kuimarisha taswira ya Tume ya Madini mbele ya wananchi.

Mafunzo hayo ya siku mbili yamehusisha watumishi kutoka idara na vitengo mbalimbali vya Tume ya Madini.




No comments:

Post a Comment