
Na Sixmund Begashe - Morogoro
Mradi wa Kurejesha Mifumo ya Chakula na Matumizi Bora ya Ardhi ( Food System, Landuse and Restoration Project - FOLUR), unaotekelezwa na Wizara ya Maliasili na Utalii unatarajiwa kuwanufaisha watanzania waliopo Bara na Visiwani, kupitia kilimo cha mpunga kwa kuzingatia matumizi bora ya ardhi na mazingira. Mradi utaimarisha usimamizi wa rasilimali za misitu na kurejesha uoto wa asili.
Hayo yamebainishwa Mkoani Morogoro na Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Misitu na Nyuki Bw. Daniel Pancras, alipokuwa akifungua kikao kazi cha watekelezaji wa mradi huo kutoka pande zote mbili za Muungano.
Bw. Pancras amesema kuwa, mradi huo ni matokeo chanya ya utekelezaji wa kazi za Serikali ya Awamu ya Sita, chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kuwaletea maendeleo watanzania na uhifadhi endelevu wa rasilimali misitu.
"Mradi huu ni wa wananchi, kama watekelezaji, hakikisheni mnawashirikisha vyema wananchi katika hatua zote zinazo wahusu, mkatangulize uzalendo ili malengo yaliyokusudiwa yafikiwe kwa haraka na kwa mafanikio makubwa". Alisema Bw. Pancras.
Aidha, aliwasisitizia watekelezaji mradi huo kuhakikisha matokeo ya mradi yaendane na thamani ya fedha zilizotolewa, ili uwe endelevu na kuacha alama yakudumu kiuchumi na kiuhifadhi.
Akizungumzia kikao kazi hicho cha siku mbili, Mratibu mradi huo Bw. Wanjala Mgaywa amesema lengo la kikao hicho ni kupata uelewa wa pamoja wa utekelezaji wa mpango kazi mradi wa mwaka 2025/2026.
Naye Afisa Mazingira kutoka Idara ya Mazingira ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais Zanzibar, Bi. Mariam Hassan Juma licha ya kuipongeza jitihada hizo za serikali, amesema, mradi huo situ utawanufaisha kiuchumi wakazi wa Mkoa wa Kusini Magharibi bali wananchi wote wa Zanzibar.
Mradi huo unaolenga kuendeleza kilimo, Matumizi bora ya Ardhi, na urejeshaji wa uoto, unatekelezwa katika Halmashauri ya Wilaya ya Mlimba, Mkoani Morogoro, na Mkoa wa Kaskazini Unguja, Zanzibar kwa zaidi ya dola za kimarekani Milioni 7.



No comments:
Post a Comment