
WAZIRI wa Ujenzi, Abdallah Ulega, ameeleza kuridhishwa na ujenzi wa barabara ya Ruanda -Idiwili mkoani Songwe unaotekelezwa na wakandarasi wanawake waliopata fursa maalumu kutokana na maelekezo ya Rais Samia Suluhu Hassan.
Mradi wa ujenzi wa barabara hiyo yenye urefu wa takribani kilomita 20 na thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 45.3, wamepewa wanawake hao kupitia Umoja wa Wakandarasi Wanawake Tanzania (TWCA) ili kuonyesha uwezo wao na kama wataifanya vizuri, watapewa pia miradi mingine.
Waziri Ulega amesema kwa muda mrefu wanawake walikuwa wakitumika zaidi katika shughuli za kusafisha barabara lakini Rais Samia ameamua kufanya uamuzi wa kimkakati ili wanawake sasa wafanye kazi kubwa zaidi na zenye kipato zaidi.
“Ninawaomba fanyeni kazi akina Mama, Mheshimiwa Rais anatambua mchango wenu na hawa wananchi wanataka kuiona barabara yao inakamilika kwa wakati ili kusudi waweze kuitumia kwa ajili shughuli za maendeleo”, amesema Ulega.
Waziri Ulega ambaye alikuwa katika ziara ya ukaguzi wa maendeleo ya ujenzi wa barabara hiyo, alieleza kufurahishwa na kasi yake aliwahakikishia kuwa Rais Samia anatambua mchango wa wakandarasi wanawake na ndio maana ameridhia kutoa fedha kwa ajili ya kuwawezesha wanawake kujenga barabara hiyo.
Aidha, Waziri Ulega amesisitiza suala la fursa za ajira kwa vijana wa eneo hilo ambalo mradi unatekelezwa na kufurahishwa na utoaji wa ajira kwa mradi huo kwa vijana na kuwataka kutolifanyia mchezo agizo hilo
“Kama wapo vijana wanaoweza kufanya kazi lazima wapewe kazi za kufanya, ni muhimu sana wakimaliza kufanya kazi muwape vyeti vya kuonesha kuwa walifanya kazi hizo ili kazi zingine zinapokuja wajulikane kwamba hawa waliwahi kufanya kazi”, ameongeza Ulega.
Kwenye suala la uwezeshaji vijana katika ujenzi, Ulega alisema msisitizo wa serikali ni kuhakikisha wanafanya kazi si za vibarua tu bali pia kupitia kampuni ndogo zinazoweza kupewa kazi za ujenzi.
Amewataka Mameneja wa TANROADS Mkoa wa Songwe na Mbeya, kuhakikisha wanawasimamia Wakandarasi hao na kutokuwepo kwa makosa madogo madogo ili ujenzi wa barabara hiyo uende kwa kasi na kukamilika kwa wakati uliokusudiwa.
Kwa upande wake, Mbunge wa Vwawa Japhet Hasunga amemuomba waziri huyo kuwa wakandarasi hao wapewa kazi ya kukamilisha kilometa 79 zilizobakia endapo watakakamilisha kipande cha kilometa hizo 20 mnamo Agosti 2026.
Akitoa taarifa ya mradi huo, Rais wa Chama cha Wakandarasi Wanawake Tanzania, Mhandisi Judith Odunga, amesema ujenzi wa barabara hiyo unafadhiliwa na Serikali ya Tanzania kwa gharama ya shilingi Bilioni 45.3.






No comments:
Post a Comment