VYUO VYA MAENDELEO YA JAMII VINAWAJIBU WA KUANDAA WAHITIMU WENYE UWEZO WA KUJITEGEMEA – MARYPRISCA - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Sunday, December 14, 2025

VYUO VYA MAENDELEO YA JAMII VINAWAJIBU WA KUANDAA WAHITIMU WENYE UWEZO WA KUJITEGEMEA – MARYPRISCA



Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Mhe. Mhandisi Maryprisca Mahundi, amesema vyuo vya maendeleo ya jamii vina wajibu wa kuandaa wahitimu wenye uwezo wa kujitegemea, kuajiri wengine na kuwa chachu ya mabadiliko chanya katika jamii zao.

Mhe. Maryprisca ameyasema hayo tarehe 13 Desemba 2025 wakati akizungumza na wanachuo pamoja na watumishi wa Chuo cha Maendeleo ya Jamii Ruaha kilichopo mkoani Iringa, akibainisha kuwa elimu inayotolewa katika vyuo hivyo inaendana na mahitaji ya nchi na inawalenga wahitimu kuwa waajirika, wajiajiri na wawezeshaji wa maendeleo ya jamii.

Ameeleza kuwa vyuo vya maendeleo ya jamii ni mhimili muhimu wa mabadiliko ya fikra, uundaji wa ajira na ustawi wa wananchi, hasa katika ngazi ya msingi ambako changamoto nyingi za kiuchumi na kijamii huanzia. Kwa mujibu wake, mwelekeo huo ni suluhisho la kupunguza utegemezi, kuongeza uzalishaji na kuimarisha ushiriki wa wananchi katika kujiletea maendeleo yao wenyewe.

Aidha, Naibu Waziri huyo amepongeza Chuo cha Maendeleo ya Jamii Ruaha kwa mafanikio ya kudahili wanafunzi 2,571 ndani ya kipindi cha miaka minne, akisema hatua hiyo inaonesha mchango mkubwa wa chuo hicho katika kuandaa rasilimali watu yenye tija kwa Taifa.

Kwa upande wake, Mkuu wa Chuo cha Maendeleo ya Jamii Ruaha, Godfrey Mafungu, amesema chuo kinaendelea kutoa mafunzo yanayolenga kuwaandaa wanafunzi kuwa watatuzi wa changamoto za jamii kwa kuunganisha nadharia na vitendo.

Amesema kupitia programu za kitaaluma, tafiti na miradi ya uzalishaji mali, chuo kimefanikiwa kuwajengea wanafunzi ujuzi unaowawezesha kuajirika, kujiajiri na kuchangia maendeleo ya jamii wanazotoka.

Akizungumza kwa niaba ya wanafunzi, Rais wa Serikali ya Wanafunzi wa chuo hicho, Abasi Kibwana Jumanne, ameishukuru Wizara pamoja na uongozi wa chuo kwa kuweka mazingira bora ya kujifunzia, akisema elimu inayotolewa inalenga zaidi ujuzi wa vitendo na mahitaji halisi ya jamii.

Amesema ziara ya Naibu Waziri imeongeza ari na motisha kwa wanafunzi katika kujifunza na kuwatumikia wananchi kwa weledi pindi watakapohitimu, huku wakiahidi kusoma kwa bidii, kuzingatia maadili na kutumia elimu wanayoipata kuwa chachu ya maendeleo katika jamii zao.


Chanzo ni WMJJWM Iringa








No comments:

Post a Comment