Bodi yatakiwa kutembelea miradi ya maji - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Friday, January 30, 2026

Bodi yatakiwa kutembelea miradi ya maji



Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji Mhandisi Mwajuma Waziri ameitaka Bodi ya Taifa ya Maji kutembelea miradi ya maji inayotekelezwa kwa lengo la kuongeza uelewa kuhusu Sekta ya maji.

Ametoa maelekezo hayo katika kikao cha kwanza cha Bodi ya Tano (5) ya Taifa ya Maji katika ukumbi wa Wizara ya Maji Mtumba jijini Dodoma.

Amesisitiza kuwepo na ushirikishwaji kati ya Bodi hiyo na Wizara ya Maji katika uandaaji wa miradi.

Amesema wajumbe wamebeba dhamana ya kuhakikisha wananchi wanapata huduma ya majisafi na salama na mafanikio yapo katika kushirikiana na kupanga kwa pamoja .

“Maji ndio kichocheo cha ukuaji wa nchi kama ilivyo elezwa kwenye Dira ya Maendeleo ya 2050 kuhusu suala la maji katika kuboresha maisha ya wananchi na Taifa kwa ujumla hivyo ni muhimu kuhakikisha malengo hayo yanafikiwa”, Mhandisi Mwajuma amesema.

Amewataka wajumbe kuwa mabalozi wazuri katika shughuli mbalimbali zinazofanywa na Sekta katika kutunza,kuhifadhi,kugawa na kusimamia Rasilimali za maji 

Mhandisi Mwajuma amesema upungufu wa maji huathiri jamii, mifugo na Kilimo hivyo ni vyema kuwa na mipango mkakati kukabiliana na changamoto za upungufu wa maji katika vyanzo vya maji.

Amewashukuru na kuwapongeza wajumbe wa bodi hiyo kwa kuaminiwa na Waziri wa Maji Mhe Jumaa Aweso (Mb) na amewaahidi kupokea ushauri na ushirikiano kwa lengo la kutangaza Sekta ya Maji na dhamira ya kumtua "mama ndoo ya maji kichwani"

Mwenyekiti wa Kamati hiyo Bwn.Hussein Sufiani Ally amesema Bodi hiyo itatoa ushikiano na maoni katika masuala mbalimbali ikiwemo utafutaji wa vyanzo vya fedha za ujenzi wa miradi ya maji na uthibiti wa upotevu wa maji.

No comments:

Post a Comment