
SERIKALI imetangaza mpango kabambe wa kuboresha miundombinu ya usafirishaji kwa njia ya barabara wenye lengo la kurahisisha usafiri, kuongeza ufanisi na kukuza Pato la Taifa.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam , Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega, amesema mpango huo unaojulikana kwa jina la Expressways Master Plan sasa umeanza kutekelezwa na wataalamu wazalendo wa Tanzania kwa kushirikiana na wenzao kutoka Korea Kusini.

Waziri Ulega amesema kwa sasa wataalamu wa pande zote wanakutana katika mafunzo maalumu ambayo yatatengeneza dira ya nini kitaenda kutokea kupitia mkakati huo kabambe.
“Tunashirikiana na wenzetu kutoka Korea Kusini ambao tayari wamepiga hatua kubwa katika eneo la miundombinu ya barabara. Leo nimefungua mkutano wa mafunzo ambao wataalamu wetu na wa Korea wanakutana kuangalia utekelezaji wa mradi huo na kutoa mafunzo kwa watu wetu.
“ Lengo letu ni kwamba kupitia mafunzo haya, wataalamu wetu watapata ujuzi utakaowawezesha kujua namna ya kupanga, kutekeleza na kuendesha miradi mikubwa kabisa ya barabara,” alisema Ulega.
Katika hotuba yake ya ufunguzi wa mafunzo hayo ya Mpango Kabambe wa Usafirishaji wa Haraka na Uwezeshaji Rasilimali watu uliofanyika jijini Dar es Salaam, ukiwashirikisha wadau mbalimbali wakiwemo wataalamu kutoka Wizara ya Ujenzi na Wakala wa Barabara Nchini (TANROADS) pamoja viongozi kutoka serikali za Korea na Tanzania, Waziri Ulega amesisitiza kuwa serikali imedhamiria kuboresha miundombinu yake usafirishaji ili iendane na wakati na mahitaji halisi ya wananchi.
Kwa mujibu wa malengo ya mkakati huo kabambe, serikali imepanga kuhakikisha kwamba shoroba zote tisa za barabara nchini zinaunganishwa kwa barabara pana zaidi, zenye mfumo wa kidijitali, zinazohimili changamoto za kimazingira na zitakazosaidia maeneo ya uzalishaji kuunganishwa na masoko na bandari.
Aidha Mhe Ulega ameipongeza serikali ya Korea kupitia kampuni ya KOICA kwa uamuzi wake wa kuijengea uwezo Tanzania ili iweze kutekeleza miradi ya ujenzi wa miundombinu ya usafiri wa haraka kwa ufanisi na kusisitiza kuwa utekelezaji wake utasaidia kutatua changamoto nyingi zinazoikabili sekta ya usafirishaji ikiwemo suala la foleni na uchakavu wa miundombinu.
“Ndugu washiriki, Tanzania ina bahati kubwa ya kupata fursa ya kujifunza kutoka kwa wenzetu Wakorea ambao kwao kusafiri kutoka mji mmoja ulioko umbali wa kilomita 400 kwenda mji mwingine kwa muda mfupi si jambo la ajabu, nichukue fursa hii kuwahakikishia kuwa sasa ni zamu yetu kutekeleza miradi ya aina hiyo ili kuwapunguzia wananchi adha ya kutumia muda mrefu kusafiri jambo ambalo linaathiri utekelezaji wa shughuli za maendeleo” aliongeza Mhe Ulega.
Pia Waziri Ulega amelitumia jukwaa la ufunguzi wa mkutano huo kuwasihi wataalamu katika sekta ya ujenzi kuhakikisha wanapata ujuzi wa kubuni, kusimamia na kutekeleza ujenzi wa miradi inayoendana na malengo ya Dira ya Taifa ya mwaka 2050.
Kwa upande wake Meneja wa Miradi ya Ubia Kati ya Sekta Binafsi na Serikali (PPP)
Mhandisi Elibariki Mkumbo amesema ili kuhakikisha malengo ya serikali kuelekea Uchumi wa kati wa juu yanafikiwa kupitia mradi huo hivi karibuni itaanza utekelezaji wa mradi wa mpango kabambe wa usafiri wa haraka kati ya Kibaha na Morogoro hatua ambayo amesema italeta Mapinduzi makubwa katika maboresho ya miundombinu ya usafirishaji nchini.
Mhandisi Mkumbo ameongeza kuwa serikali kwa kushirikiana na kampuni ya KOICA kutoka Korea Kusini imeanza mpango wa kuwajengea uwezo wataalamu wake katika sekta ya ujenzi ikiwemo TANROADS ili waweze kupata ujuzi stahiki wa kutekeleza miradi hiyo kwa tija.




No comments:
Post a Comment