
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Ridhiwan Kikwete,akizungumza na waandishi wa habari Januari 30, 2026 jijini Dodoma.
Na Okuly Julius, OKULY BLOG, DODOMA
Waajiriwa wapya katika Utumishi wa Umma wametakiwa kuripoti katika vituo vyao vya kazi ndani ya siku 14 tangu kupokea barua za kupangiwa vituo, la sivyo nafasi zao zitachukuliwa na wasailiwa wengine waliopo kwenye kanzidata ya Sekretarieti ya Ajira.
Akizungumza na waandishi wa habari Januari 30, 2026 jijini Dodoma, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Ridhiwan Kikwete wakati akielezea utekelezaji wa ahadi ya siku 100 za Serikali ya Awamu ya Sita, kipindi cha pili cha uongozi wa Rais Dkt Samia Suluhu Hassan katika utumishi wa umma, amesema maelekezo hayo yanahusu waajiriwa wote wapya waliopangiwa vituo vya kazi katika ajira za hivi karibuni.
Waziri Kikwete amesema Serikali imetoa kibali cha ajira kwa jumla ya nafasi 12,000, zikiwemo ajira 7,000 za kada ya elimu (ualimu) na ajira 5,000 za kada ya afya, ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa ahadi za Mheshimiwa Rais ndani ya siku 100 za Serikali ya Awamu ya Sita.
Ameeleza kuwa kibali hicho cha ajira kilitolewa baada ya Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuapishwa tarehe 3 Novemba 2025.
Amebainisha kuwa kwa mujibu wa Kifungu cha 7, Kifungu kidogo cha 7 cha Sheria ya Utumishi wa Umma, Sura ya 298, jukumu la kuendesha mchakato wa ajira katika Utumishi wa Umma linatekelezwa na Sekretarieti ya Ajira iliyo chini ya Ofisi ya Rais.
Amesema baada ya tangazo la ajira kutolewa na maombi kupokelewa, Sekretarieti ya Ajira iliratibu usaili uliofanyika katika mikoa yote ya Tanzania Bara pamoja na vituo maalum vya Unguja na Pemba.
Aidha, amesema kuwa usaili wa mchujo (Aptitude Test) ulifanyika kwa njia ya kidigitali kati ya tarehe 13 na 14 Desemba 2025, na matokeo ya usaili huo yalitolewa siku hiyo hiyo. Usaili wa mahojiano kwa waombaji wote waliofaulu ulifanyika baadaye.
Waziri Kikwete ameongeza kuwa Sekretarieti ya Ajira iliwapangia vituo wasailiwa wote waliofaulu kati ya tarehe 11 hadi 20 Januari 2026, ambapo barua za kupangiwa vituo zilitumwa moja kwa moja kwenye akaunti za waombaji, badala ya utaratibu wa awali wa kufuata barua hizo jijini Dodoma.
Akizungumzia hatua ya uripoti kazini, amesema kuwa hadi sasa jumla ya watumishi 8,416 wameripoti katika halmashauri mbalimbali nchini, wakiwemo watumishi 3,694 wa kada ya elimu na watumishi 4,722 wa kada ya afya.
Amebainisha kuwa kufuatia maelekezo ya Rais Samia Suluhu Hassan kwamba watumishi watakaoripoti mapema waingizwe kwenye orodha ya mishahara, jumla ya watumishi 735 walioripoti kabla ya kufungwa kwa orodha ya mishahara waliingizwa kwenye payroll ya Serikali na tayari wamelipwa mishahara yao katika mwezi wa kwanza wa mwaka 2026.
Ameongeza kuwa bado watumishi 956 wa kada ya elimu pamoja na watumishi wa kada ya afya wapo kwenye mchakato wa kujaza nafasi zilizobaki, ambapo nafasi hizo tayari zimetangazwa na usaili unaendelea. Amesema watumishi wote wataingizwa kwenye payroll ya Serikali kulingana na muda watakaoripoti katika vituo vyao vya kazi.

No comments:
Post a Comment