DKT. ASHATU KIJAJI: HALI YA UTALII NCHINI IKO IMARA, MAPATO YAPAA - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Friday, January 16, 2026

DKT. ASHATU KIJAJI: HALI YA UTALII NCHINI IKO IMARA, MAPATO YAPAA


Na Sixmund Begashe, DSM


Waziri wa Malia asili na Utalii Dkt. Ashatu Kijaji amewataka wadau wa uhifadhi na utalii kujipanga ipasavyo katika utoaji wa huduma zinazokidhi viwango vya kimataifa ili Taifa liweze kunufaika na jitihada za Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania za kuinyanyua sekta ya uhifadhi na utalii. 

Dkt. Kijaji ameyasema hayo Jijini Dar es Salaam kwenye mahafali ya 23 ya Chuo cha Taifa cha Utalii na kuongeza kuwa Sekta ya utalii na ukarimu inahitaji ujuzi utakaosaidia kutoa huduma bora na yenye ushindani na kwamba sekta hiyo inatoa ajira takriban milioni 1.5 za moja kwa moja na zisizo za moja kwa moja kila Mwaka.

Kuhusu hali ya Utalii nchini Dkt. Kijaji amesema hali ya utalii nchini kwa sasa iko imara na inaendelea kuimarika ambapo takwimu za kuanzia mwezi Januari hadi Novemba mwaka 2025, zinaonesha idadi ya Watalii imeongezeka kwa asilimia 9.02 ambapo kwa mujibu wa Ripoti ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT) ya mwezi Oktoba, mapato yatokanayo na utalii yamefikia Dola za Kimarekani bilioni 4.2, kiwango cha juu zaidi kuwahi kufikiwa katika historia ya nchi yetu. 

Aidha, Dkt. Kijaji ametaka kuwepo na jitihada za makusudi za kuboresha eneo la ukarimu kutokana na eneo hilo kuwa na fursa za kimkakati za kupunguza ushindani na kukuza Utalii ili kufikia viwango vya kimataifa na kufikia lengo la watalii milioni 8 na kuongeza mapato ifikapo mwaka 2030 kama ilivyoelekezwa kwenye Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2025.

Akizungumza wakati wa kumkaribisha Mgeni rasmi, Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii Dkt. Hassan Abbasi amesema soko la ajira ni kubwa na fursa katika sekta ya Utalii iko vizuri na wazi ambapo wahitimu wanaweza kuchagua kujiajiri ama kuajiriwa kutokana na sekta hiyo kuwa mtambuka na kuwataka wahitimu kuchangamkia fursa zilizopo katika sekta hiyo. 

Awali, akizungumza katika mahafali hayo Mkuu wa Chuo cha Taifa cha Utalii Dkt. Florian Mtei amesema chuo hicho kina jumla ya kampasi nne nchini kote na kuzalisha wataalam mbalimbali wakiwemo waongoza Utalii, wahudumu, waratibu wa shughuli na ukarimu ili kufikia azma ya Serikali ya kuwa na watalii milioni 8 ifikapo mwaka 2030 sambamba na kuongeza ajira kwa Watanzania. 

Mahafali hayo yanehudhuriwa pia na Dkt. Thereza Mugobi, Mkurugenzi wa Utalii, Dkt. Edward Kohi Mkurugenzi wa Utafiti na Mafunzo pamoja na Wadau wa sekta ya Utalii ambapo jumla ya wanafunzi 674 wametunukiwa vyeti mbalimbali.

No comments:

Post a Comment