DKT. LEKASHINGO AONGOZA KIKAO CHA KAMISHENI YA TUME YA MADINI, AWEKA MSISITIZO MIKAKATI YA KUVUKA LENGO LA MADUHULI - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Friday, January 30, 2026

DKT. LEKASHINGO AONGOZA KIKAO CHA KAMISHENI YA TUME YA MADINI, AWEKA MSISITIZO MIKAKATI YA KUVUKA LENGO LA MADUHULI


Na Mwandishi Wetu - Dodoma


Mwenyekiti wa Tume ya Madini, Dkt. Janet R. Lekashingo, ameongoza kikao cha Kamisheni ya Tume ya Madini kilichofanyika leo Januari 30, 2026 jijini Dodoma, kikilenga kupokea na kujadili taarifa ya utekelezaji wa majukumu ya Tume kwa kipindi cha miezi mitatu, sambamba na kuweka mikakati thabiti ya kuimarisha mchango wa Sekta ya Madini katika ukuaji wa uchumi wa nchi.

Kikao hicho, kilichowakutanisha Makamishna wa Tume pamoja na Menejimenti, kimeweka msisitizo kwenye uboreshaji wa usimamizi wa shughuli za uchimbaji na biashara ya madini, ukusanyaji wa maduhuli, uendelezaji wa masoko ya madini pamoja na kudhibiti utoroshaji wa madini, hatua zinazolenga kuongeza mchango wa Sekta ya Madini kwenye Pato la Taifa.

Baada ya kupokea taarifa kutoka kwa Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini, Mhandisi Ramadhani Lwamo, pamoja na taarifa za Wenyeviti wa Kamati za Tume, Dkt. Lekashingo amepongeza mafanikio yaliyopatikana, hususan katika eneo la ukusanyaji wa maduhuli, usimamizi wa masoko ya madini na vituo vya ununuzi vilivyoanzishwa nchini, kuimarika kwa usalama kwenye shughuli za uchimbaji, ushirikishwaji wa Watanzania katika Sekta ya Madini pamoja na mchango wa kampuni za madini kwa maendeleo ya jamii.

Aidha, Mwenyekiti huyo ameitaka Menejimenti kuendelea kubuni na kutekeleza mikakati bunifu ya kuongeza mapato ya Serikali kupitia vyanzo mbalimbali, ili kuiwezesha Tume ya Madini kuvuka lengo la kukusanya Shilingi trilioni 1.2 lililowekwa kwa mwaka wa fedha 2025/2026.

Katika kikao hicho, changamoto mbalimbali zinazoikabili Sekta ya Madini zimejadiliwa kwa kina na kuwekewa mikakati ya utekelezaji kupitia Kamati za Ufundi, Rasilimali Watu, Fedha na Ushirikishwaji wa Watanzania katika Sekta ya Madini. Lengo ni kuhakikisha wachimbaji wanafanya kazi katika mazingira rafiki na salama, yanayowawezesha kujipatia kipato endelevu huku Sekta ya Madini ikiendelea kuwa nguzo muhimu ya uchumi wa nchi.

Hatua hizo zinaonesha dhamira ya Tume ya Madini kuendelea kuisimamia sekta hiyo kimkakati, kwa maslahi mapana ya taifa na ustawi wa wananchi.

No comments:

Post a Comment