SERIKALI YASISITIZA KUTOA HATIMILIKI KWA WANANCHI WOTE WENYE SIFA - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Friday, January 30, 2026

SERIKALI YASISITIZA KUTOA HATIMILIKI KWA WANANCHI WOTE WENYE SIFA


Serikali imesema itahakikisha kila mwananchi mwenye sifa za kumiliki ardhi anapata hatimiliki yake kwa wakati, huku ikiwataka watendaji wa sekta ya ardhi kuacha urasimu na kushirikiana na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kuwaletea wananchi maendeleo na furaha.

Akizungumza na wananchi waliojitokeza kwenye Kliniki Maalum ya Ardhi inayoendelea katika Ofisi za Ardhi Mkoa wa Dodoma, tarehe 28 Januari 2026, Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mheshimiwa Caspal Muya (Mb.), amesema ni muhimu kuhakikisha wananchi waliokamilisha taratibu za umiliki wanapatiwa hatimiliki zao bila kucheleweshwa, akibainisha kuwa wapo waliokuwa wakisubiri kwa muda mrefu.

“Nitasimamia kuhakikisha kila mwananchi mwenye uhalali wa kumiliki ardhi anapata hatimiliki yake kwa wakati,” amesema Naibu Waziri Muya.

Amesema ili kuboresha utoaji wa huduma, amewaagiza wataalamu wa sekta ya ardhi nchini kutoa elimu kwa wananchi kuhusu matumizi bora ya ardhi na taratibu za kupata hatimiliki, akieleza kuwa hatua hiyo itasaidia kuzuia ujenzi holela unaokiuka mipango ya matumizi ya ardhi.

Mheshimiwa Muya ameongeza kuwa Serikali ya Awamu ya Sita imedhamiria kusimamia haki ya umiliki wa ardhi kwa vitendo na kuhakikisha wamiliki halali wanapatiwa hatimiliki zao.

Ameeleza kuwa Serikali inayoongozwa na Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, itaendelea kusogeza huduma za utoaji wa hatimiliki karibu na wananchi katika maeneo mbalimbali nchini.

Aidha, amesema Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi chini ya Waziri wake, Mheshimiwa Dkt. Leonard Akwilapo, imeweka mkakati wa siku 14 kuhakikisha kila mwananchi wa Jiji la Dodoma aliyekidhi vigezo vya kupata hatimiliki anapatiwa hati yake, hatua itakayorahisisha huduma na kulinda haki za wananchi.

Awali, Katibu Mkuu wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mhandisi Anthony Sanga, amesema wamiliki wa ardhi waliokamilisha taratibu zote wanapaswa kupewa hatimiliki zao bila maneno mengi, akiwataka watumishi wa sekta hiyo kuondoa urasimu katika utekelezaji wa zoezi hilo.

Mhandisi Sanga amesisitiza kuwa ni marufuku kwa mtumishi wa sekta ya ardhi kumwelekeza mwananchi mwenye uhitaji wa huduma kwenda kwa mtu mwingine, akieleza kuwa atasimamia msimamo huo kwa kuwa mwananchi anahitaji huduma kwa wakati.

Katika siku ya kwanza ya zoezi hilo, zaidi ya hatimiliki 20 tayari zimetolewa, huku zaidi ya 100 zikiwa katika hatua za mwisho za kukamilishwa.

No comments:

Post a Comment