Na Mwandishi Wetu
Wadau na wawekezaji mbalimbali wameonesha nia ya kuwekeza katika sekta ya mafuta nchini Tanzania, uwekezaji ambao utachangia ukuaji wa uchumi wa nchi na kuboresha huduma ya bidhaa za nishati kwa wananchi.
Miongoni mwa wawekezaji hao ni Kampuni ya Mafuta ya India (Indian Oil Corporation Limited), yenye uzoefu mkubwa katika usambazaji wa mafuta na gesi, ambayo imeonesha nia ya kuwekeza nchini Tanzania.
Kampuni hiyo imeonesha nia hiyo katika kikao kilichofanyika kati yao na ujumbe wa Tanzania ukiongozwa na Naibu Waziri wa Nishati, Mhe. Salome Makamba pembezoni mwa Maadhimisho ya Wiki ya Nishati ya India 2026 yanayoendelea Jimbo la Goa, nchini India.
Katika kikao hicho, Mkurugenzi wa Mipango na Biashara wa kampuni hiyo, Suman Kumar, amesema Tanzania ni soko la bidhaa nyingi ikiwemo bidhaa za nishati.
Amesema kutokana na ongezeko la mahitaji ya bidhaa kama mafuta, gesi ya mitungi na nishati linalotokana na ukuaji wa uchumi, idadi ya watu inayoongezeka na miji kukua haraka, inatoa fursa kwa kampuni za nishati kushirikiana katika usambazaji, uchakataji na huduma za nishati.
Kwa upande wake Mhe. Salome amesema “Serikali ya Tanzania inawakaribisha wawekezaji wote na ipo wazi kwa uwekezaji wa kimataifa katika sekta ya nishati, ikiwa ni pamoja na usambazaji wa mafuta na gesi ya mitungi kuendana na msukumo wa Serikali wa kukuza matumizi ya nishati safi ya kupikia."
Aidha Mhe. Salome amewahimiza wawekezaji hao kuona umuhimu wa kufungua matawi nchini Tanzania na kushiriki katika ununuzi wa pamoja wa bidhaa za mafuta ili kuongeza ushindani na uhakika wa upatikanaji wa mafuta ya gharama nafuu nchini.
"Hivyo tunawakaribisha wadau wote kuja kuwekeza nchini Tanzania kupitia makubaliano ya kibiashara na kampuni zetu za ndani kulingana na sera za Tanzania na mapendekezo ya wawekezaji” amesema Mhe. Salome.
Maadhimisho ya Wiki ya Nishati ya India 2026 yanatarajiwa kuhitimishwa Januari 30, 2026 na yamewakutanisha washiriki kutoka nchi zaidi ya 125, yakivutia wawekezaji wengi wa kigeni katika sekta ya nishati.
Kupitia Maadhimisho hayo yamefungua fursa mbalimbali za uwekezaji katika sekta ya nishati kwa wadau na wawekezaji kutoka sehemu mbalimbali duniani.






No comments:
Post a Comment