
Na OWM - TAMISEMI
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OWM–TAMISEMI) Mhe. Prof. Riziki Shemdoe ameitaka Manispaa ya Morogoro kuona uwezekano wa kujenga sehemu maegesho ya magari pembezoni mwa Mradi wa Stendi ya Mabasi Madogo ya Kihonda inayojengwa kupitia mradi wa TACTIC, ili maegesho hayo yawe ni chanzo kipya cha mapato ya manispaa hiyo.
Prof. Shemdoe ametoa wito huo kwa uongozi wa Manispaa ya Morogoro, mara baada ya baada ya kumaliza ukaguzi wa ujenzi wa mradi wa Stendi ya Mabasi Madogo Kihonda, stendi ambayo inajengwa karibu na Stesheni ya SGR ya Jakaya Kikwete Morogoro.
“Kuna watu wanatoka mbali wanakuja Stesheni ya Jakaya Kikwete ili waende Dar es Salaam na kurudi jioni lakini wakifika hapo stesheni wanakuta maegesho ya magari yamejaa, hivyo manispaa jengeni maegesho ya magari ambayo yatawaingizia kipato,” ameelekeza Prof. Shemdoe.
Prof. Shemdoe aitaka Manispaa hiyo ya Morogoro kushirikiana na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Morogoro ili kurahisisha mchakato wa ujenzi wa magesho ya magari ambayo yatakuwa ni chanzo kipya cha mapato ndani ya mkoa wa Morogoro.
“Ombeni eneo litakalowawezesha kujenga maegesho ya magari, mimi nina watu wengi kwenye magrupu ya WhatsApp wanalalamika kukosa sehemu ya kupaki magari yao pindi wanapotaka kusafiri na treni ya mwendokasi (SGR),” amesisitiza Prof. Shemdoe.
Ameongeza kuwa, ujenzi wa mradi wa maegesho ya magari utakuwa ni mradi fungamanishi na mradi wa Ujenzi wa Stendi Ndogo ya Mabasi Kihonda pamoja na mradi wa Kitaifa wa Kimkakati wa Treni ya Umeme (SGR).
Aidha, Prof. Shemdoe ameipongeza Manispaa ya Morogoro kwa utekelezaji mzuri wa Mradi wa Ujenzi wa Stendi ya Mabasi Madogo Kihonda na kuwataka kuwa na fikra za kubuni miradi fungamanishi kama wa maegesho ya magari ili ufungamane kiutendaji na mradi wa Kimkakati wa Treni ya Umeme (SGR).
Akitoa taarifa ya utekelezaji wa Mradi huo wa stendi, Mratibu Msaidizi wa Mradi wa TACTIC Mkoa wa Morogoro, Mhandisi Mboka Nkwera amesema stendi hiyo itakuwa na daraja kubwa litakalounganisha Stesheni ya Jakaya Kikwete na Jengo Kuu la Stendi, ambalo litatumiwa na abiria wa treni ya SGR.
Mradi huo wa ujenzi wa Stendi ya Mabasi Madogo Kihonda unatekelezwa na mkandarasi M/S TIL Constrution Limited na unajengwa kwenye eneo lenye ukubwa wa mita za mraba 55,723.32 kwa gharama ya Shilingi 1,743,927,140.00 na unatarajiwa kukamilika Julai 21, 2026.





No comments:
Post a Comment