
Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar (Mb), akizungumza wakati wa kikao na Uongozi wa Benki ya Maendeleo ya Afrika Mashariki (EADB), ambacho kilizungumzia mambo mbalimbali kuhusu benki hiyo pamoja na kujadili fursa za ushirikiano kati ya Serikali na Benki hiyo hasa katika fursa za mikopo kwa taasisi za umma na sekta binafsi, kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Waziri wa Fedha, Treasury Square, jijini Dodoma.

Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Benki ya Maendeleo ya Afrika Mashariki (EADB), Dkt. Charles Mwamwaja ambaye aliongoza ujumbe wa benki ya EADB, akitoa maelezo ya awali ya benki hiyo kwa Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar (Mb) (hayupo pichani), walipomtembelea ofisi kwake Treasury Square, jijini Dodoma, ambapo walizungumza mambo mbalimbali kuhusu benki hiyo pamoja na kujadili fursa za ushirikiano kati ya Serikali na Benki hiyo hasa katika fursa za mikopo kwa taasisi za umma na sekta binafsi.

Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Benki ya Maendeleo ya Afrika Mashariki (EADB), Bw. Benard Mono akifafanua jambo wakati wa kikao cha Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar (Mb), (hayupo pichani) na uongozi wa benki hiyo, kilichofanyika ukumbi wa mikutano wa Waziri wa Fedha, Treasury Square, jijini Dodoma.

Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar (Mb), akiongoza kikao kati yake na Uongozi wa Benki ya Maendeleo ya Afrika Mashariki (EADB) ambapo walizungumza mambo mbalimbali kuhusu benki hiyo pamoja na kujadili fursa za ushirikiano kati ya Serikali na Benki hiyo, Treasury Square, jijini Dodoma.

Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar (Mb) (wa tano kulia), Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Benki ya Maendeleo ya Afrika Mashariki (EADB), Dkt. Charles Mwamwaja (wa tano kushoto), Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, Bi. Amina Khamis Shaaban (wa tatu kulia), Kamishna wa Idara ya Fedha za Nje, Bw. Rished Bade (watatu kushoto), Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Benki ya Maendeleo ya Afrika Mashariki (EADB), Bw. Benard Mono (wa nne kulia), Meneja Mkazi wa Benki ya Maendeleo ya Afrika Mashariki (EADB), Bw. Stephen Wambura (wa nne kushoto) na maafisa wengine waandamizi wa Wizara ya Fedha, wakiwa katika picha ya pamoja baada ya kikao chao kilichojadili mambo mbalimbali kuhusu Benki ya EADB pamoja na kujadili fursa za ushirikiano kati ya Serikali na Benki hiyo hasa katika fursa za mikopo kwa taasisi za umma na sekta binafsi.
(Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, WF, Dodoma)
Na. Farida Ramadhani na Silya Kombe, WF, Dodoma
Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar ameishauri Benki ya Maendeleo ya Afrika Mashariki (EADB) kuongeza ubunifu katika kushirikiana na Serikali pamoja na Sekta binafsi ili kuchangia katika maendeleo ya nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Ametoa ushauri huo jijini Dodoma alipokutana na kuzungumza na uongozi wa benki hiyo kuhusu masuala mbalimbali ya maendeleo ikiwa ni pamoja na fursa za ushirikiano kati ya Serikali na benki hiyo, katika Ofisi za Wizara ya Fedha, Treasury Square.
Mhe. Balozi Omar alisema kuwa benki hiyo ni muhimu katika maendeleo ya nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki na ikitumika vizuri inaweza kuufanya Ukanda huo kuwa mfano wa ukuaji wa maendeleo ya kiuchumi na kijamii barani Afrika.
“Kasi ya maendeleo yanayotokana na benki hiyo ikionekana vizuri tutakuwa wa mfano na kuiwezesha jumuiya nyengine kama Jumuiya ya Kiuchumi ya Nchi za Afrika Magharibi (ECOWAS) na Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) kuja kujifunza kwetu”, alibainisha Mhe. Balozi Omar.
Aidha alisema kuwa ni muhimu pia kwa benki hiyo kuchangia katika kupunguza umaskini ikiwa ni pamoja na kujenga ujuzi na ustadi unaoendana na mahitaji ya kiuchumi, na mipango ya maendeleo ya muda mfupi na mrefu.
Aliishauri pia benki hiyo kujitangaza ili kuwawezesha wananchi hususan Sekta Binafsi waweze kutambua fursa mbalimbali zinazo patikana katika benki hiyo.
“ Jukumu lenu ni kuhakikisha wateja wanaifahamu zaidi benki pamoja na fursa zake”, alisisitiza Mhe. Balozi Omar.
Aidha, aliipongeza benki hiyo kwa mipango na michango mbalimbali ambayo imekuwa ikichangia katika maendeleo ya nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki hasa Tanzania.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Benki ya Maendeleo ya Afrika Mashariki (EADB), Dkt. Charles Mwamwaja, alisema benki hiyo ilianzishwa mwaka 1967 kwa lengo la kuchangia katika kukuza maendeleo ya kiuchumi na wananchi wa nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Alisema benki hiyo imeandaa mkakati madhubuti wa kuwawezesha wadau kufahamu fursa mbalimbali zinazopatikana katika benki hiyo kwa kuwa benki hiyo haifanyi kazi na Serikali pekee bali hata sekta ninafsi katika kuleta maendeleo.
Aidha, aliahidi kuyafanyia kazi kikamilifu maaelekezo na ushauri uliotokewa na Mhe. Waziri ili kuwezesha nchi kukamilisha mipango yake na kufikia maendeleo ya kiuchumi na ustawi wa wananchi.
Naye Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Benki ya Maendeleo ya Afrika Mashariki (EADB), Bw. Benard Mono, alisema kuwa benki hiyo ipo tayari kuendeleza ushirikiano na Serikali ya Tanzania katika miradi ya maendeleo ili kuzalisha ajira na kuongeza thamani katika sekta mbalimbali za uzalishaji.
Bw. Mono aliongeza kuwa wapo tayari kutoa mikopo katika sekta za umma pamoja na sekta binafsi kwa kuzingatia vigezo vya mkopeshwaji kwa lengo la kujenga Uchumi imara kwa nchi za Afrika Mashariki ikiwamo Tanzania, kama lilivyo lengo la benki hiyo kuanzishwa la kuchochea maendeleo.
Kikao hicho kilihudhuriwa pia na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, Bi. Amina Khamis Shaaban, Kamishna wa Idara ya Fedha za Nje, Bw. Rished Bade, Meneja Mkazi wa Benki ya Maendeleo ya Afrika Mashariki (EADB), Bw. Stephen Wambura na maafisa wengine waandamizi wa Wizara ya Fedha.

No comments:
Post a Comment