TAASISI YA SUBRA NA NUSRA WAANDAA KONGAMANO MAALUMU LIKILENGA KUWAANDAA WANAWAKE KIROHO NA KIJAMII - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Saturday, January 31, 2026

TAASISI YA SUBRA NA NUSRA WAANDAA KONGAMANO MAALUMU LIKILENGA KUWAANDAA WANAWAKE KIROHO NA KIJAMII

 


Na Oscar Assenga,

Kutokana na kuporomoka  mmomonyoko wa maadili katika jamii, wanawake wa Kiislamu mkoani Tanga wameanzisha majadiliano na mikakati maalum ya kutafuta suluhisho la changamoto hiyo, sambamba na maandalizi ya kuupokea mwezi mtukufu wa Ramadhani.


Kupitia Taasisi ya Subra na Nusra, wanawake hao wameandaa kongamano maalum litakalofanyika Jumamosi hii katika Ukumbi wa Simba Mtoto, jijini Tanga, likilenga kuwaandaa wanawake kiroho na kijamii ili kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia mafundisho ya Mtume Muhammad (SAW).


Mratibu wa kongamano hilo, Bi Mwanakombo Abdallah Kipanga, alisema lengo kuu ni kutoa elimu kwa jamii, hususan wanawake, kuhusu umuhimu wa maadili mema na maandalizi sahihi ya mwezi wa Ramadhani.



“Huu si mwezi wa kawaida. Tunataka wanawake wapate elimu itakayowasaidia kuimarisha imani, malezi ya watoto na maadili ndani ya familia na jamii kwa ujumla,” alisema.

Alisema Mufti Abubakar Bin Zuberi anatarajiwa kuwa mgeni wa heshima, huku Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Balozi Dk Batilda Burian, akiwa mgeni rasmi. Hili litakuwa kongamano la nne kufanyika chini ya taasisi hiyo.

Bi Kipanga aliongeza kuwa jitihada hizo zimeungwa mkono pia na wanawake wenye asili ya Tanga wanaoishi Dar es Salaam, walioungana kuimarisha maandalizi ya kongamano hilo.


Miongoni mwa mada zitakazojadiliwa ni maandalizi ya wanawake katika mwezi wa Ramadhani, kujenga hofu ya Mungu, malezi bora ya watoto pamoja na umuhimu wa kuzingatia maadili mema katika maisha ya kila siku.


Aliwataka wanawake wa Kiislamu pamoja na wa dini nyingine kujitokeza kwa wingi kushiriki kongamano hilo.
Naye mjumbe wa kamati ya maandalizi, Bi Shamsi Diwani kutoka Dar es Salaam, alisema kuna haja ya dharura kwa wanawake kuungana kupambana na kuporomoka kwa maadili kunakojitokeza katika jamii.


“Ni wakati wa kusaidiana kurejesha maadili mema. Inasikitisha kuona mienendo isiyofaa na burudani zinazokiuka maadili zikizidi kushika kasi katika jamii,” alisema.


Aliongeza kuwa wako tayari kukaa pamoja na wanawake na kujadili kwa kina chanzo cha changamoto hiyo ili kupata suluhisho la kudumu.


Bi Diwani pia alielezea wasiwasi wake juu ya kuongezeka kwa migogoro ya ndoa na kuvunjika kwa familia, akisema si jambo jema kushuhudia baadhi ya wanawake wakisherehekea talaka.


“Hili si jambo la kufurahia. Ingawa talaka inaruhusiwa, si tukio la kushangiliwa,” alisisitiza.
Kwa upande wake, Bi Kibibi Saidi Kibao aliwahimiza wanawake kuhudhuria ili kunufaika na mafunzo yatakayotolewa na Mashehe maarufu pamoja na mke wa Mufti wa Kwanza, Sheikh Jumaa.

Naye mjumbe mwingine wa kamati, Bi Hawa Mweri, alisisitiza umuhimu wa wanawake wa Kiislamu kudumisha maadili mema wakati wote, si kipindi cha Ramadhani pekee.
MWISHO

No comments:

Post a Comment