UJUMUISHAJI WA HUDUMA ZA FEDHA NI MUHIMU AFRIKA MASHARIKI – BoT - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Thursday, January 29, 2026

UJUMUISHAJI WA HUDUMA ZA FEDHA NI MUHIMU AFRIKA MASHARIKI – BoT


Naibu Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Bi. Sauda Msemo, amesema kuwa ujumuishaji wa huduma za fedha na ulinzi wa watumiaji wake ni nguzo muhimu katika kuimarisha sekta za fedha na kufikia maendeleo jumuishi na endelevu kwa wananchi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Bi. Msemo ameyasema hayo wakati wa ufunguzi wa warsha inayofanyika tarehe 28 hadi 30 Januari 2026 katika Tawi la Benki Kuu ya Tanzania, Arusha, ukiwakutanisha wajumbe kutoka Benki Kuu za nchi za Afrika Mashariki.

Alisisitiza kuwa mkutano huo ni jukwaa muhimu la kujadili na kuratibu mikakati ya pamoja ya kuongeza upatikanaji na matumizi ya huduma jumuishi za fedha pamoja na kuwalinda watumiaji wa huduma hizo, hatua itakayosaidia kupunguza umaskini na kuongeza ustawi wa wananchi wa ukanda huo.

Aliongeza kuwa washiriki wa mkutano wanapaswa kujikita katika kutatua changamoto zinazokwamisha matumizi ya huduma rasmi za fedha, hususan kwa makundi ya wanawake, vijana, watu wenye ulemavu na wafanyabiashara wadogo, akibainisha kuwa makundi hayo ni muhimu katika kufikia maendeleo jumuishi na endelevu.

Akizungumza awali, Mkurugenzi wa Ustawi na Huduma Jumuishi za Fedha, Bw. Kennedy Komba, alisema kuwa kupitia kamati hiyo, nchi wanachama zitaweza kuunda sera bora kwa kutumia taarifa zilizoratibiwa, mifumo ya vipimo na kazi ya uchambuzi wa pamoja, huku wakihakikisha kuwa ustawi wa watumiaji, ustahimilivu wa kifedha na ukuaji jumuishi vinaendelea kuwa nguzo kuu za ajenda ya ujumuishaji wa sekta ya fedha katika Afrika Mashariki.

Aidha, alisema kuwa majadiliano ya kitaalamu katika mkutano huo yanajikita katika maeneo muhimu yakiwemo huduma jumuishi za fedha, viwango vya taarifa, mfumo wa vipimo vya afya ya kifedha (financial health), ulinzi wa watumiaji wa huduma za fedha, usimamizi wa mwenendo wa soko, elimu ya fedha pamoja na ubunifu jumuishi wa fedha unaoibuka kikanda na duniani.

Majadiliano hayo yanalenga kuonesha umuhimu wa kuanzishwa kwa Kamati ya Wataalamu wa Huduma Jumuishi za Fedha na Ulinzi wa Watumiaji wa Huduma za Fedha, itakayosaidia kushughulikia masuala ya mshikamano wa kiuchumi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki katika eneo la ujumuishaji wa huduma za fedha na ulinzi wa watumiaji wake.

No comments:

Post a Comment