Na Gideon Gregory - Dodoma
Inaelezwa kuwa katika vitongoji vingi ambavyo tayari vimeonja huduma ya umeme hapa nchini, mabadiliko makubwa yameanza kuonekana, katika Kijiji cha Chihikwi Mkoani Dodoma, mashine zimeanza kuchukua nafasi ya kazi ngumu za mikono, huku vijana wakianza kuona sababu ya kubaki vijijini badala ya kuhamia mijini.
Hali hiyo inatokana na kasi ya Serikali katika kusambaza nishati ya umeme katika vitongoji vyote nchini.
Mwishoni mwa juma lililopita Januari 17,2026 Serikali kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA) ilisaini mikataba 30 yenye thamani ya shilingi Trilioni 1.2 kwa ajili ya kutekeleza Mradi wa kusambaza umeme katika Vitongoji 9,009 unaotarajiwa kunufaisha wateja wa awali 290,300 katika mikoa 25 ya Tanzania Bara.
Hatua hiyo ya Serikali inafungua ukurasa mpya wa matumaini kwa wananchi, huku umeme ukionekana kuwa mtaji muhimu wa kukuza pato la mwananchi mmoja mmoja na kila kaya nchini.
Jeremiah Peter ni Mkazi wa Kijiji cha Chihikwi, anasema kabla ya umeme kupatikana katika eneo lao maisha yalikuwa magumu kwasababu walishindwa kujiajiri, licha ya kujishughulisha na kilimo pamoja na uchomaji mkaa.
"Sasa hivi kwakuwa umeme umekuja moja ya changamoto ambazo zilikuwa zinatukabili kama hizo za ajira kwasasa zimetatulika na vijana wengi tumeweza kuchangamkia fursa kama kuchomelea, kufungua saluni za kunyoa na maduka ya kuchajia simu,"anasema.
Tofauti na mtazamo wa awali wa kupeleka umeme kwa ajili ya matumizi ya nyumbani pekee, mkataba huu unaweka msisitizo kwenye kuunganisha nishati na uzalishaji wa kiuchumi kama biashara ndogo ndogo, viwanda vidogo, usindikaji wa mazao na huduma za kijamii.
Kwa mtazamo wa kiuchumi, umeme huleta mapinduzi ya moja kwa moja katika tija ya kazi ambapo mashine zinazotumia umeme hupunguza muda wa kazi, gharama za uzalishaji na uchovu wa nguvu kazi.
Hatua hiyo inaelezwa na Mchambuzi wa masuala ya kiuchumi Joel Kasasa kama hatua ya mwanzo ya kujenga mnyororo wa thamani wa uchumi wa ndani kuanzia ngazi ya chini.
"Mkataba huu wenye thamani ya Trilioni 1.2 wa kufikia vitongoji 9,009 Tanzania bara utawezesha na utachochea kasi ya ukuaji wa uchumi pengine kufikia kiwango cha Umoja wa Mataifa cha malengo ya maendeleo endelevu (SDGs), hasa lile engo namba Saba la kuhakikisha kwamba ifikapo 2030 tunakuwa tumewafikia watu wengi na nishati, "anasema.
Bwana Kasasa anafichua kuwa hata yale mataifa ambayo yamekuwa yakiingia kwenye migogoro ya kiuchumi ni kwasababu ya kutafuta udhibiti katika eneo la nishati, kwasababu taifa lililo imarika katika eneo hilo lina uhakika wa kuzalisha kwa kiwango linachotaka ikiwa na maana ya kushinda sokoni.
Mama lishe anayehifadhi vyakula kwenye friji, kijana anayefungua karakana ya umeme, au mkulima anayesindika mazao yake hapo hapo kijijini wote hawa wanashuhudia ukweli mmoja kuwa umeme unapowafikia uzalishaji huongezeka, na mapato huanza kupanda.
Hapa ndipo dhana ya “umeme kama mtaji” inapoanza kuwa halisi kama ambavyo Jeremiah Peter anavyoeleza kuwa baada ya umeme kuwafikia maisha yake yamebadilika na kuwa tofauti na zamani.
"Huduma ya umeme imekuwa mwarobaini wa ajira kwa upande wetu, fursa nyingi zimeweza kujitokeza kupitia miundombinu hii ya umeme kufika katika Kijiji chetu tumeweza kujiajiri wenyewe,"anaeleze.
Naye Alfred Helmani mkazi wa Kijiji hicho cha Chihikwi anaeleza kuwa huduma ya umeme katika eneo lao imefungua fursa nyingi baada ya watu kuweza kutengeneza misingi imara ambayo imeweza kuwakwamua kiuchumi na kuongeza mapato yao.
"Kwasasa kuna watu wamefungua huduma ya kuchajisha simu, maana watu walikuwa wanachaji mbali wengine wameanzisha huduma ya kuchomelea, lakini kabla ya ujio wa huduma hii hali ilikuwa giza na fursa kama hizi hazikuwepo kama hizo za vijana kujiajiri, "anaeleza.
Katika ngazi ya Halmashauri, umeme unaanza kuonekana kama fursa ya kupanga upya uchumi wa eneo, maeneo ya viwanda vidogo, masoko, na vikundi vya wajasiriamali vinaanza kuunganishwa na nishati hii mpya.
Mwakilishi wa Serikali ya Kijiji cha Chihikwi Michael Mjeleza anakiri kuwa changamoto kubwa si kuupata umeme, bali ni kwenye uzalishaji, diyo maana mipango ya mafunzo, vikundi vya uzalishaji na ujasiriamali inawekwa ili umeme usibaki majumbani pekee.
Bwana Mjeleza anasema mipango yao kwa sasa inalenga kuunganisha umeme na masoko, vikundi vya wajasiriamali pamoja na kutenga maeneo ya uzalishaji ili kuongeza tija.
"Kuna baadhi ya vipande vya ardhi tumevitenga, endapo tutapata umeme wa uhakika tuna mpango wa kufungua viwanda ambavyo vitawawezesha vijana kujikimu na kimaisha na mahitaji yao,"anasema.
Kwa miongo mingi, maendeleo yalionekana kama jambo linalotoka juu kushuka chini. Hata hivyo leo, Serikali inaonekana kuchagua njia tofauti ya kujenga uchumi kuanzia ngazi ya vitongoji na hapa Waziri wa Nishati, Deogratius Ndejembi, anasema dhamira ya Serikali si kuwasha balbu pekee, bali kuwasha fursa za kiuchumi kwa wananchi.
Anasema "Sekta ya nishati ni injini ya kuchochea maendeleo ya taifa na jamii kwa ujumla wake, kwa kutambua hilo Mheshimiwa Rais amekuwa akitenga fedha nyingi kwa ajili ya kupeleka umeme kwa wananchi ili kuhakikisha kuwa maisha yao yanaboreshwa, ikumbukwe kuwa hakuna uchumi wa kisasa unaoweza kukua bila kuwa na nishati ya uhakika, imara, inayotabirika na gharama nafuu.
Akizungumzia utekelezaji wa Miradi mbalimbali kama hiyo Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Mhandisi Hassan Saidy anasema REA inatekeleza azma ya Serikali ya kuhakikisha umeme unawafikia Wananchi kwa vitendo.
Hivyo kufikia mwishoni mwa mwaka uliopita 2025, Serikali ilifanikiwa kufikisha umeme katika vijiji vyote 12,318 vya Tanzania Bara, hatua iliyoleta mapinduzi ya kweli ya kiuchumi na kijamii ikichangia kuboresha maisha ya Wananchi wanaoishi vijijini.
"Mwaka 2021 kati ya vitongoji 64,359 vilivyopo Tanzania Bara, vitongoji 28,258 pekee vilikuwa na umeme wakati vitongoji 36,101 vilikosa huduma hiyo muhimu,"anasema.
Katika hatua nyingine anafafanua kuwa kupitia utekelezaji wa Miradi mbalimbali kuanzia mwaka 2021 hadi Desemba 2025, Serikali iliunganisha umeme katika vitongoji 10,745, na hivyo kuongeza idadi ya vitongoji vyenye umeme kufikia 39,003.
Miaka iliyopita umeme ulionekana kama alama ya maendeleo lakini leo hii unaanza kuonekana kama chanzo cha maendeleo chenyewe.
Umeme unaowaka vitongojini hauangazi nyumba pekee, bali unaangazia mustakabali wa uchumi wa Taifa ambapo katika kila balbu inayowaka, kuna biashara inayozaliwa na kwa kila mashine inayozunguka, kuna kipato kinachoongezeka.
Safari hii, maendeleo yanaonekana kuanzia pale yalipopaswa kuanzia kwa muda mrefu ambapo ni kwa mwananchi wa kawaida.
Vitongoji 9,009 sio takwimu tu, bali ni maelfu ya safari ndogo za kiuchumi zinazoanza na katika kila safari hiyo, umeme hauwashi taa pekee, bali unawasha matumaini ya kipato na maisha bora.



No comments:
Post a Comment