
Serikali imepunguza kwa kiasi kikubwa ada za maombi ya leseni kwa vyombo vya habari mtandaoni kutoka shilingi 500,000 hadi 50,000, huku ada ya maombi ikishushwa kutoka shilingi 50,000 hadi 10,000. Hatua hiyo imetajwa kuwa mkombozi kwa wanahabari na wamiliki wa blogu nchini.
Tangazo hilo limetolewa na Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Hamis Mwinjuma maarufu kama Mwana FA, wakati akifungua rasmi Mkutano Mkuu wa Mwaka wa Vyombo vya Utangazaji ulioandaliwa na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) katika Ukumbi wa New Generation jijini Dodoma.
Mbali na kupunguza ada hizo, Mhe. Mwinjuma ameielekeza TCRA kushirikiana na Bodi ya Ithibati ili kuhakikisha wafanyakazi wa vyombo vya habari wanalipwa stahiki zao kwa wakati, wakiwemo wanaodai mishahara ya zaidi ya miezi mitano.
Amesisitiza kuwa ndani ya wiki moja anatarajia kupokea mrejesho wa hatua zilizochukuliwa kushughulikia suala hilo.
Amesema Serikali inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan itaendelea kuboresha mazingira ya ufanyaji kazi kwa vyombo vya habari, huku akisisitiza umuhimu wa ubora wa maudhui, kuzingatia maadili ya taaluma na kulinda haki miliki.
“Haki ya kupata taarifa ni ya kila Mtanzania, hivyo vyombo vya habari vinapaswa kuwafikia wananchi wote bila upendeleo,” amesisitiza.
Aidha, amesema wizara itaendelea kuimarisha mazingira ya sekta hiyo ili wananchi wa vijijini wanufaike na huduma za utangazaji kwa urahisi, sambamba na kuhimiza matumizi ya teknolojia za kisasa ikiwemo Akili Unde (AI) kwa tija.
Katika hatua nyingine, Mhe. Mwinjuma ameielekeza Kampuni ya Usambazaji wa Machapisho na Vifaa vya Utangazaji (KOSOTO) kushirikiana na TCRA kupambana na uharamia wa maudhui na kuwasilisha mrejesho ndani ya mwezi mmoja.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa TCRA, Dkt. Jabiri, ametaja takwimu za vyombo vya habari vilivyosajiliwa nchini na kuahidi kuendelea kuboresha miundombinu ya mawasiliano kwa kuzingatia Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Mkutano huo wa siku mbili, unaofanyika Februari 12 na 13, 2026, umewakutanisha viongozi na wadau wa sekta ya utangazaji kujadili namna ya kuimarisha na kupanua huduma za utangazaji nchini.




No comments:
Post a Comment