Katika Mahakama ya wilaya ya Babati Machi 25, 2026 limefunguliwa shauri la uhujumu uchumi namba 6525/2026 mbele ya Mh. Jumaa Mwambago hakimu mkazi mwandamizi wa Mahakama ya wilaya ya Babati dhidi ya aliyekuwa afisa Ardhi mteule wa Halmashauri ya mji Babati Bw. Samwel Donald Lyimo.
Mshtakiwa ameshtakiwa kwa kosa la kushindwa kukidhi matakwa ya ilani ya kueleza mali anazomiliki kwa kutoa maelezo ya uongo kuhusiana na viwanja anavyomiliki kinyume na kifungu cha 26(3) cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa sura ya 329, marejeo ya 2023 kikisomwa pamoja na aya ya 21 ya Jedwali la kwanza na vifungu vya 57(1) na 61(2) vya sheria ya kudhibiti uhujumu uchumi na makosa ya kupangwa, sura ya 200 marejeo ya 2023.
Akisoma hati ya mashtaka, mwendesha mashtaka wa TAKUKURU Bi. Neema Gembe ameeleza kuwa mshtakiwa akiwa mtumishi wa umma kama Afisa Ardhi mteule wa Halmashauri ya mji wa Babati alishindwa kukidhi matakwa ya ilani ya kuelezea mali anazomiliki kwa kutoa maelezo ya uongo kuhusu viwanja anavyomiliki.
Mshtakiwa amekana kutenda kosa hilo, aidha alishindwa kutekeleza masharti ya dhamana na kupelekwa magereza. Shauri liliahirishwa hadi Machi 26, 2026 ili kusikiliza maombi ya dhamana dhidi ya mshtakiwa.


No comments:
Post a Comment