
Balozi wa Tanzania nchini Zimbabwe, Kamishna wa Polisi (CP) Suzan Kaganda, ameshiriki mdahalo wa viongozi waandamizi uliofanyika katika Chuo Kikuu cha Zimbabwe, jijini Harare ambapo Mdahalo huo ulikuwa na kaulimbiu isemayo “Uhuru wa Kimkakati: Kusawazisha Maslahi ya Afrika katika Mabadiliko ya Kijiografia na Kisiasa.”
Mdahalo huo uliwakutanisha viongozi waandamizi wa Serikali ya Zimbabwe, wanadiplomasia, wachumi na wanasiasa kutoka maeneo mbalimbali nchini humo, Washiriki walipata fursa ya kubadilishana uzoefu na kujadili mikakati ya kulinda na kuendeleza maslahi ya bara la Afrika katika mazingira ya mabadiliko ya kisiasa na kiuchumi duniani.
Katika mdahalo huo, Mheshimiwa Kaganda aliwasilisha mada kuhusu mchango wa Tanzania katika kuimarisha ushirikiano wa kikanda kupitia uanachama wake katika Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) na Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), akieleza kuwa Tanzania imeendelea kuwa mhimili muhimu katika kukuza mshikamano wa kikanda na maendeleo ya pamoja barani Afrika.
Aidha, alibainisha kuwa Tanzania imekuwa mfano bora kwa nchi wanachama wa SADC kwa kuwekeza katika ujenzi wa miundombinu ya kisasa ambapo aliitaja miradi hiyo kama vile barabara, reli ya kisasa (SGR), pamoja na upanuzi wa bandari kuwa imeongeza ufanisi wa usafirishaji na kuifanya Tanzania kuwa lango muhimu la biashara katika ukanda wa Kusini mwa Afrika.
Katika hatua nyingine, Mheshimiwa Kaganda alifanya mazungumzo na Kaimu Mkuu wa Idara ya Elimu na Utafiti wa Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine (SUA), Profesa Maulid Matawala, ambaye yuko nchini Zimbabwe kwa ziara ya kikazi. Mazungumzo yao yalijikita katika kuimarisha ushirikiano katika sekta ya elimu ya juu kati ya Tanzania na Zimbabwe.
Vilevile Profesa Matawala anatarajiwa kukutana na viongozi wa vyuo vikuu mbalimbali vya Zimbabwe, ikiwemo Chuo Kikuu cha Zimbabwe (UZ), kwa lengo la kujadili fursa za ushirikiano katika elimu, utafiti na ubadilishanaji wa wataalamu.



No comments:
Post a Comment