WAZIRI MKUU Dkt. Mwigulu Nchemba ametoa majibu ya mgogoro wa ardhi baina ya wakazi wa Wilaya ya Monduli na Jeshi la Wananchi ambao umedumu tangu mwaka 2004 baada ya kumpigia simu Mkuu wa Majeshi nchini na kumweleza kilio cha wanaMonduli.
Waziri Mkuu alichukua hatua hiyo jana jioni (Ijumaa, Machi 6, 2026) wakati akizungumza na wananchi na viongozi mbalimbali kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika katika uwanja wa Barafu Mto wa Mbu, wilayani Monduli, mkoani Arusha.
Akitoa majibu baada ya maongezi yao, Dkt. Mwigulu aliwaeleza wananchi hao kwamba Mkuu wa Majeshi nchini ameridhia hoja yao iliyotolewa na Mbunge wa Monduli, Isack Joseph pamoja na Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM, Namelok Sokoine ambao waliomba suala la fidia lisiwepo bali wananchi waachiwe kuendelea kushirikiana na jeshi kama ilivyokuwa zamani.
“Mkuu wa Majeshi ameridhia kwamba hakuna jambo la fidia. Makubaliano mliyokuwa nayo awali ya mafunzo na malisho yaendelee vilevile. Bali ametoa angalizo kwamba watu wasijenge makazi ya kudumu kama mlivyokubaliana awali,” alisema na kuamsha nderemo na shangwe kutoka kwa wananchi hao.
Waziri Mkuu alitoa rai kwa watendaji wa Halmashauri nchini akiwataka waheshimu na kulinda maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya malisho ya mifugo ili kuepusha migogoro na kuhakikisha shughuli za ufugaji zinaendelea kwa tija. “Maeneo yanayohusu wafugaji tusiyadokoe, tusiyachanganye. Tuendelee kulinda maeneo ya wafugaji bila kuyachanganya na matumizi mengine.”
Mapema, Mbunge wa Monduli, Isack Joseph alimuomba Waziri Mkuu afuatilie suala hilo ili wanaotaka kumilikishwa eneo hilo kwa kudai fidia, wasipatiwe hiyo fursa bali libakishwe kuwa eneo huru kwa Jeshi la Wananchi na kwa wafugaji. Eneo hilo lina kilometa za mraba 870 ambazo ni sawa na ekari 214,981.68
Pia alimuomba afuatilie suala la malipo ya mabomba ya maji kwenye kiwanda cha Pipes Industries ambacho kinatengeneza mabomba kwa ajili mradi wa maji wa vijiji 13 vya Monduli wenye thamani ya sh. bilioni 20.3. Mradi huo unatarajiwa kutoa maji umbali wa km. 45 kutoka Ngaramtoni hadi Monduli mjini.
Vilevile, mbunge huyo alieleza changamoto zinazoikabili sekta ya utalii katika eneo la Mto wa Mbu kwamba licha ya kuwa eneo hilo lina vivutio vikubwa vya utalii, bado linasimamiwa kama Game Controlled Area, jambo linalosababisha watalii wengi kukwepa kulitembelea na hivyo kudhoofisha uchumi wa wilaya hiyo.
Naye, Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM, Namelok Sokoine akisisitiza kuhusu eneo hilo alisema anakubaliana na maelezo ya Mbunge wake, Bw. Isack Joseph kwa vile anatambua kuwa wafugaji hawana mbadala zaidi ya mifugo yao. “Kitu pekee ambacho wazazi wetu wanaweza kutuachia kama urithi ni mifugo na ardhi yetu,” alisema.
Alisema kwamba marehemu baba yake (hayati Edward Moringe Sokoine) alitambua umuhimu wa ardhi na malisho ndipo aliamua kutenga eneo la jeshi kufanyia mafunzo lakini pia ambalo wafugaji wangeweza kulisha mifugo yao pale. “Nia yake kubwa ni ili maeneo yale yasiweze kuuzwa kwa watu wengine, njia pekeee ilikuwa ni kuwapa jeshi walitumie kwa mafunzo lakini pia wafugaji walitumie wakati hakuna mafunzo.”
Alisema kuwa mwaka jana kupitia kwa mbunge wao mstaafu, Fredrick Lowassa, walikuwa na vikao virefu na Waziri wa Ulinzi kuhusu suala hilo na wakaazimia kuwa hawako tayari kufidiwa kwa kuwa hawana mahali pengine pa kwenda.
“Sisi wafugaji hatuna pa kupeleka mifugo yetu. Tunajua kuwa ardhi haiongezeki licha kuwa watu na wanyama wanaongezeka; na kokote mtakapotupeleka, tunatambua kuwa migogoro ya ardhi haiishi. Ndiyo maana tulisema tulisema tungependa kubaki katika eneo letu. Serikali itambue tunatamani tubaki pale. Wana Monduli tunasema hatuko tayari kufidiwa, tunaomba tuendelee kubaki katika ardhi yetu na tuko tayari kubakia na Jeshi,” alisisitiza.






No comments:
Post a Comment