MRADI WA MALAGARASI WAPELEKA UMEME KWA KAYA 750 KIGOMA - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Saturday, March 7, 2026

MRADI WA MALAGARASI WAPELEKA UMEME KWA KAYA 750 KIGOMA


Takribani kaya 750 zinazopitiwa na Mradi wa Uzalishaji Umeme wa Malagarasi (MW 49.5) unaotekelezwa mkoani Kigoma zimefaidika na mradi huo, ikiwa ni jitihada za Serikali kuhakikisha kuwa wananchi wanaopitiwa na miradi ya maendeleo wananufaika na miradi husika.

Naibu Waziri wa Nishati, Mhe. Salome Makamba amewasha umeme katika Kitongoji cha Mdyandelema, Kata ya Kazuramimba, Wilaya ya Uvinza mkoani Kigoma, ambacho ni miongoni mwa vitongoji 18 vilivyowashiwa umeme kupitia mradi huo.

Akizungumza na wananchi mara baada ya kuzindua huduma hiyo ya umeme, Mhe. Salome amesema utekelezaji wa mradi huo ni maagizo ya Rais, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ambaye ameielekeza Wizara ya Nishati kuhakikisha kuwa ifikapo mwaka 2030 vitongoji vyote viwe vimesambaziwa umeme.


Kutokana na hilo, Mhe. Salome amewataka wananchi kutunza miundombinu ya umeme ili kuunga mkono lengo la Rais Samia la kuifanya Kigoma kuwa kitovu cha umeme, hasa baada ya kukamilika kwa kituo kikubwa cha kupoza umeme cha Kidahwe kitakachokuwa na uwezo wa megawati 192, ambacho kitakuwa ngome ya kusambaza umeme katika mikoa ya Magharibi.

Katika hatua nyingine, Mhe. Salome amesema gharama ya kuunganishiwa umeme vitongojini ni shilingi 27,000 tu ambapo amesisitiza kuwa hata kama mwananchi ametandaza nyaya za umeme katika sehemu ya nyumba yake, bado anastahili kuunganishiwa huduma hiyo.

Kuhusu nishati safi ya kupikia, Mhe. Salome amewaasa wananchi kutumia majiko ya umeme, majiko banifu na mitungi ya gesi kwa ajili ya kupikia. Pia ameutaka Wakala wa Nishati Vijijini (REA) pamoja na TANESCO kuhakikisha wanatoa elimu ya matumizi ya nishati hiyo kwa wananchi hadi ngazi ya vitongoji.

Mkuu wa Wilaya ya Uvinza, Dinah Mathamani, kwa upande wake amemshukuru Rais, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuukumbuka Mkoa wa Kigoma katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo, ikiwemo ya nishati.

Amesema hapo awali hali ya upatikanaji wa umeme ilikuwa haitabiriki, lakini sasa huduma hiyo imeimarika na kuwa ya uhakika, hali inayowawezesha wananchi kufanya shughuli za biashara, kupata mwanga pamoja na kutumia umeme kwa kupikia na hivyo kusaidia kuhifadhi mazingira.

Kwa upande wake, Mwakilishi wa Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati (Umeme na Nishati Jadidifu), Mhandisi Edson Ngabo amesema mradi wa Malagarasi unahusisha sehemu tatu ambazo ni ujenzi wa bwawa la kuzalisha umeme, njia ya kusafirisha umeme msongo wa kv 132 na upelekaji wa umeme katika vijiji saba vyenye vitongoji 18 pamoja na utekelezaji wa miundombinu mingine ikiwemo ujenzi wa barabara ya lami, hospitali na shule.

Ameongeza kuwa mradi huo tayari umeshaunganisha umeme katika vijiji saba vyenye vitongoji 18 kwa gharama ya shilingi bilioni 6.8.

No comments:

Post a Comment