DUWASA YAANZA MATENGENEZO BAADA YA BOMBA LA MAJITAKA KUBOMOKA DODOMA - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Sunday, March 15, 2026

DUWASA YAANZA MATENGENEZO BAADA YA BOMBA LA MAJITAKA KUBOMOKA DODOMA



Na Okuly Julius, OKULY BLOG, DODOMA


Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dodoma (DUWASA) imeanza mara moja kushughulikia changamoto iliyojitokeza baada ya bomba kubwa la majitaka lenye kipenyo cha milimita 760 kubomoka katikati ya barabara inayotoka Singida kuelekea Dar es Salaam katika eneo la Chako ni Chako jijini Dodoma, hali iliyosababisha usumbufu wa usafiri na kulazimu vyombo vya usafiri kuelekezwa kutumia barabara mbadala.

Meneja wa Kitengo cha Majitaka na Usafi wa Mazingira DUWASA, Mhandisi Ores John, amesema kuwa mamlaka hiyo inashirikiana na wataalamu kutoka Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) kuhakikisha matengenezo yanafanyika haraka ili kurejesha huduma ya usafiri katika barabara hiyo muhimu.

Amesema maandalizi yote muhimu, ikiwemo kupeleka mitambo na vifaa vya kazi katika eneo husika, yamekamilika na kazi ya ukarabati imeanza rasmi kwa lengo la kurejesha hali ya kawaida kwa haraka ili wananchi waendelee na shughuli zao za kila siku.

Kwa mujibu wa Mhandisi John, kazi hiyo inatarajiwa kukamilika ndani ya siku saba endapo hakutajitokeza changamoto nyingine zaidi ya zilizopo kwa sasa.

Wakati huo huo, baadhi ya wananchi wameiomba Serikali kuharakisha ufunguzi wa barabara ya mzunguko ya nje ya Jiji la Dodoma ili magari makubwa ya mizigo yaweze kuitumia, hatua ambayo itasaidia kupunguza msongamano na adha ya usafiri katika maeneo ya katikati ya Jiji.



No comments:

Post a Comment