
Na Mwandishi Wetu - Dar es Salaam
Kuelekea maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani yanayoadhimishwa Machi 8 kila mwaka, wanawake wa Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL) wametoa msaada wa vifaa mbalimbali kwa watoto wenye matatizo ya moyo wanaopatiwa matibabu katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) jijini Dar es Salaam.
Msaada huo umetolewa Machi 7, 2026 ikiwa ni sehemu ya shughuli za kijamii zinazofanywa na wanawake wa TTCL katika kuadhimisha siku hiyo muhimu kwa wanawake duniani.
Akizungumza kwa niaba ya MWENYEKITI wa Kamati ya wanawake TTCL, Afisa Uhusiano Mwandamizi, Bi. Adeline Berchimance,amesema lengo la msaada huo ni kuonesha mshikamano, upendo na kuwapa faraja watoto wanaopatiwa matibabu ya moyo pamoja na wazazi na walezi wao wanaokaa hospitalini kwa muda mrefu wakiwahudumia.
Amesema wanawake wa TTCL wameona ni muhimu kufika katika taasisi hiyo ili kushiriki na jamii katika kipindi cha maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani kwa kutoa msaada na faraja kwa watoto wanaokabiliwa na changamoto za kiafya.
“Tunafahamu kuwa safari ya matibabu si rahisi kwa watoto hawa pamoja na wazazi wao.
Ndiyo maana leo tumekuja si tu na msaada wa vifaa, bali pia na ujumbe wa faraja na matumaini kwa familia hizi,” amesema Bi. Adeline.
Miongoni mwa vifaa vilivyotolewa ni pamoja na pampas (diapers) kwa watoto, maziwa kwa watoto wachanga pamoja na pedi (taulo za kike) kwa wazazi na walezi wanaokaa hospitalini kwa muda mrefu wakihudumia watoto wao.
Bi. Adeline amesema msaada huo umeandaliwa kwa kuzingatia mahitaji halisi ya watoto wanaopatiwa matibabu katika taasisi hiyo pamoja na changamoto wanazokutana nazo wazazi na walezi wanapokuwa hospitalini kwa muda mrefu.
Aidha, amewapongeza madaktari, wauguzi na wataalamu wa afya wa JKCI kwa kazi kubwa wanayoifanya ya kuokoa maisha ya watoto na kuwapa matumaini mapya familia nyingi nchini.
Amesema huduma wanazozitoa wataalamu hao ni muhimu sana kwa Taifa kwa kuwa zinachangia kuokoa maisha ya watoto wengi wenye matatizo ya moyo.






No comments:
Post a Comment