MAJI WASHIRIKIANA NA SEKTA BINAFSI KUENDELEZA VYANZO VYA MAJI - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Thursday, March 26, 2026

MAJI WASHIRIKIANA NA SEKTA BINAFSI KUENDELEZA VYANZO VYA MAJI


Sekta ya Maji inaendelea kuwashirikisha wadau wa maendeleo na sekta binafsi katika kufanikisha miradi mbalimbali ya maji kwa manufaa ya jamii.

Moja ya wadau hao ambao wameshirikishwa katika utunzaji wa vyanzo vya maji ni kampuni ya vinywaji baridi ya Coca cola.

Kampuni hiyo imewekeza Dola za Marekani milioni 1.94 kwa utekelezaji wa mradi wa uhifadhi wa vyanzo vya maji katika Kidakio cha Ngerengere, katika Bonde la Wami-Ruvu mkoani Morogoro.

 Kaimu Mkurugenzi wa Rasilimali za Maji Wizara ya Maji, Bi. Rosemary Rwebugisa, amesema mradi huo unaendana na mkakati wa Wizara ya Maji wa kuimarisha uhifadhi wa vyanzo vya maji na kuhakikisha upatikanaji endelevu wa rasilimali hiyo kwa maendeleo ya jamii na uchumi.

Amesema wakulima pamoja na maelfu ya wananchi wa Manispaa ya Morogoro, Mvomero na Morogoro Vijijini watanufaika na mradi huo, kwa kulinda chanzo muhimu kinachohudumia Mkoa wa Pwani na Jiji la Dar es Salaam.

Bi. Rwebugisa amebainisha kuwa Wizara ya Maji itaendelea kushirikiana na wadau wa maendeleo, sekta binafsi na jamii katika kutekeleza miradi ya uhifadhi wa vyanzo vya maji, sambamba na kujenga uelewa wa matumizi endelevu ya Rasilimali za Maji.

 Amesisitiza kuwa ushirikiano huo ni sehemu ya juhudi za serikali za kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi na kuhakikisha usalama wa maji kwa vizazi vya sasa na vijavyo.

Meneja Rasilimali Watu na Utawala wa Bodi ya Maji ya Bonde la Wami-Ruvu Bw. Juvenalis Tarimo kwa niaba ya Mkurugenzi wa Bodi hiyo amesema taasisi hiyo itaendelea kusimamia na kulinda rasilimali za maji kwa kuzingatia sheria za usimamizi wa Rasilimali za Maji ili kuhakikisha mradi huo unaleta tija kwa jamii yote.

Mradi huo utatekelezwa katika eneo la Ngerengere ndani ya Bonde dogo la Ruvu ukihusisha pia kujenga uwezo kwa jamii katika usimamizi endelevu wa rasilimali za maji pamoja na kuhamasisha matumizi ya mbinu bora za kilimo kinachostahimili mabadiliko ya tabianchi.

Mradi huo unaongozwa na mashirika ya Shirika la Global Water Challenge (GWC) na International Union for Conservation of Nature (IUCN), Coca-Cola Tanzania pamoja na Bodi ya Maji ya Bonde la Wami- Ruvu ukiwa sehemu ya jitihada za pamoja za kulinda vyanzo vya maji na kuimarisha maisha ya wananchi.

No comments:

Post a Comment