Na Mwandishi Wetu, OKULY BLOG - DODOMA.
Mgogoro wa ardhi uliodumu kwa takribani miaka 15 kati ya familia ya marehemu na mnunuzi wa shamba, Abeid Mohamed Mbelengo, hatimaye umefikia mwisho kwa amani baada ya kupatiwa suluhu kupitia Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia (Samia Legal Aid Campaign).
Bi. Hawa Sandari Kalimeje, mkazi wa Dar es Salaam na mjane wa marehemu aliyekuwa mmiliki wa shamba hilo, anasema mgogoro huo ulianza baada ya kifo cha mume wake mwaka 2013, kufuatia kutokea kwa migogoro ya mirathi ndani ya familia.
Anasema wakati wa mazishi ya mume wake kijijini mkoani Mtwara, hakujua kuwa sehemu ya shamba la familia ilikuwa tayari imeuzwa na mmoja wa watoto wa marehemu.
“Niliporudi ndipo nikapewa taarifa kuwa shamba limeuzwa na aliyelinunua tayari alikuwa amejenga ukuta mkubwa. Hali hiyo ilinisononesha sana kwa sababu sikupewa taarifa yoyote,” alisema Bi. Hawa.
Kwa mujibu wa maelezo yake, shamba hilo lilikuwa na ukubwa wa takribani hekari 15, lakini baada ya kifo cha mume wake baadhi ya watoto wa familia waliendelea kuuza sehemu za ardhi huku mgogoro ukiendelea.
Bi. Hawa anasema kwa muda mrefu aliendelea kuhangaika kutafuta haki yake hadi mwaka 2025 aliposikia kuhusu Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia na kufika katika Wizara ya Katiba na Sheria kuwasilisha malalamiko yake.
“Nilisikilizwa na kutiwa moyo. Waliifuatilia kesi yangu kwa karibu hadi tukafikia muafaka. Nimepata haki yangu bila kutumia gharama yoyote,” alisema
Kwa upande wao, wasimamizi wa mirathi wakiongozwa na Kanduru Mussa Kanduru walisema mgogoro huo uliwatesa kwa muda mrefu huku wakihangaika katika vyombo vya sheria bila kupata suluhisho la haraka.
Alieleza kuwa baada ya kifo cha ndugu yao Machi 15, 2013, watoto wa marehemu walimteua dada yao kuwa msimamizi wa mirathi, lakini baadaye migogoro ilizuka na kusababisha wazazi wa familia kuteuliwa kuchukua nafasi hiyo.
“Kwa zaidi ya miaka 11 tulikuwa tukizunguka mahakamani bila kupata suluhisho la kudumu. Kupitia msaada wa kisheria wa serikali hatimaye mgogoro ulimalizika kwa maelewano na kila mmoja akapata haki yake,” alisema Kanduru.
Kwa upande wake, mnunuzi wa shamba hilo, Abeid Mohamed Mbelengo, alisema alinunua eneo hilo mwaka 2011 kutoka kwa mmoja wa watoto wa marehemu aliyekuwa akijitambulisha kama msimamizi wa mirathi.
Alisema shauri hilo liliendelea mahakamani kwa miaka mingi hadi Wizara ya Katiba na Sheria ilipoingilia kati na kulitatua ndani ya miezi miwili kupitia vikao vitatu vya usuluhishi.
“Niliamua kuchagua amani kuliko kuendelea na mgogoro unaonyima utulivu. Niliomba nirejeshewe fedha nilizolipa na nikarejeshewa shilingi milioni 1.05 kisha nikakabidhi shamba,” alisema Mbelengo.
Kutokana na uamuzi wake wa kuacha shamba hilo kwa amani na kuepusha kuendelea kwa mgogoro, Waziri wa Katiba na Sheria, Juma Homera alimtunuku Mbelengo zawadi ya shilingi milioni 15 kama ishara ya kuthamini uzalendo na moyo wake wa kuleta amani.
Wakati huo huo, mgogoro mwingine uliomhusisha mkazi wa Dar es Salaam, Rosemary Spendi, pia ulipatiwa suluhu kupitia kampeni hiyo ya msaada wa kisheria.
Rosemary alisema alipangisha mpangaji aliyelipa kodi kwa miezi mitatu tu kati ya miezi tisa aliyokaa katika nyumba yake. Baadaye mpangaji huyo alitumia nyaraka za kughushi kwenda kukopa fedha benki kwa kutumia nyumba hiyo kama dhamana.
“Nilizunguka mahakamani kwa miaka miwili bila suluhu, kesi ikasikilizwa na mahakimu watano tofauti. Nilipofika Wizara ya Katiba na Sheria kupitia kampeni ya Mama Samia nikapatiwa msaada na hatimaye nikarudishiwa nyumba yangu,” alisema.
Akizungumza kuhusu mafanikio ya kampeni hiyo, Waziri wa Katiba na Sheria, Juma Homera, alisema wizara hiyo itaendelea kuwa kimbilio la wananchi wanaohitaji msaada wa kisheria, hasa wanyonge.
Alisema serikali inaendelea kuhimiza wananchi kutumia zaidi njia ya usuluhishi katika kutatua migogoro yao kabla ya kufikisha masuala mahakamani.
“Mgogoro unanyima watu amani na kuwazuia kufanya kazi kwa utulivu. Ndiyo maana tunasisitiza wananchi watumie kwanza usuluhishi, mahakama iwe hatua ya mwisho,” alisema.
Aliongeza kuwa kupitia Kampeni ya Samia Legal Aid zaidi ya Watanzania milioni 4.1 walipata msaada wa kisheria mwaka jana, hatua iliyosaidia kumaliza migogoro mingi na kurejesha amani katika familia na jamii.






No comments:
Post a Comment