
Na Mwandishi Wetu, Kahama
Naibu Waziri wa Nishati Mh. Salome Makamba amekabidhi vitendea kazi vya usafiri kwa TANESCO Mkoa wa Shinyanga kwa lengo la kuimarisha utoaji wa huduma kwa wananchi na kutatua changamoto zao kwa haraka.

Akizungumza tarehe 27, Machi 2026 wakati wa hafla ya kukakabidhi vitendea kazi hivyo iliyofanyika katika Manispaa ya Kahama Mkaoni Shinyaga Mhe. Salome amesema hatua hiyo ya kukabidhi vitendea kazi hivyo ni kuyaishi maono ya Mhe Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuhakikisha wananchi wanapata huduma za Umeme wa uhakika.
Amesema vitendea kazi hivyo vinakwenda kuongeza ufanisi katika utendaji kazi kwa watumishi wa TANESCO Mkoa wa Shinyanga na kuwawezesha kutatua changamoto za wateja kwa wakati.
“Kupitia vyombo hivi vya usafiri vitakwenda kuleta mabadiliko makubwa katika kumfikia mteja kwa haraka na kumhudumia, niwaombe mvitumie kutatua changamoto zao kwa wakati “ amesema Salome.
Aidha Mhe. Salome ametumia nafasi hiyo kuwataka wakazi wa Manispaa ya Kahama kuchangamkia matumizi ya Nishati safi ya umeme kupikia kwani Nishati ya umeme ni nafuu salama na rafiki kwa mazingira.
“Niwaombe wakina mama wa Kahama tuchangamkie matumizi ya nishati safi ya kupikia ya umeme, TANESCO wameleta majiko hapa unapika kwa urahisi na haraka zaidi”.
Hata hivyo Mhe. Salome amesema Serikali kupitia Shirika la Umeme TANESCO inaendelea kwa kasi kuimarisha hali ya upatikanaji wa umeme katika Manispaa ya Kahama kutokana na kuendelea kukua kwa Mji huo ambapo mpaka sasa tayari zaidi ya Shilingi milioni 600 zimetengwa kwa ajili ya kujenga laini mpya ya umeme itakayo wahudumia wakazi wa Manispaa ya Kahama.
Kwa upande wake Kaimu Meneja wa TANESCO Mkoa wa Shinyanga Mhandisi Benson Mbigili amesema wamepokea vitendea kazi mbalimbali ikiwemo Magari manne (4), Bajaji moja (1) pamoja na Pikipiki nne (4).
Mha. Benson ameipongeza Serikali kupitia Shirika la Umeme Tanzania TANESCO kwa kuwezesha vitendea kazi hivyo ambavyo kwa sasa wanakwenda kuvitumia kufikisha huduma kwa wananchi kwa haraka zaidi.
Amesema kupitia Magari hayo sasa yatawasaidia kuwafikia wateja wapya katika maeneo yote hasa yale korofi ambapo kabla ya Magari hayo ilikuwa changamoto kuwafikia na kuwaahidi wananchi kuendelea kutoa huduma bora na ya uhakika kila wakati.
“Tunaishukuru Serikali kupitia Shirika la umeme Tanzania TANESCO kwa kutupa vitendea kazi hivi ambavyo kwa sasa tunakwenda kuvitumia kufikisha huduma kwa wananchi kwa haraka zaidi.
Aidha amesema TANESCO Mkoa wa Shinyanga inaendelea kwa kasi kubwa kuhamasisha matumizi ya Nishati safi ya kupikia kwa umeme ili wananchi waweze kuelewa umuhimu wa kutumia nishati hiyo kupikia.







No comments:
Post a Comment