
Na Carlos Claudio, OKULY BLOG ,DODOMA.
Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), Mhe. Devotha Minja, amesema kamati hiyo imefanya ziara katika DUWASA kwa lengo la kukagua maendeleo ya mradi wa mtandao wa maji taka uliokuwa umesimama kutokana na kuchelewa kupatikana kwa vibali.
Akizungumza leo Machi 18, 2026 jijini Dodoma katika ziara ya kamati ya kudumu ya bunge ya hesabu za serikali (PAC) , Minja amesema kuwa vibali hivyo sasa vimepatikana na mkandarasi anatarajiwa kurejea kazini kuanza utekelezaji wa mradi huo muhimu.
Amesisitiza kuwa kamati imeelekeza kuwepo kwa ushirikiano wa karibu kati ya Wizara ya Maji na Serikali kwa ujumla ili kuhakikisha mradi huo unakamilika kwa wakati uliopangwa.

“Mkandarasi alikuwa ameondoka site kutokana na changamoto za malipo, lakini tumemhoji na ametuhakikishia kuwa baada ya malipo kukamilika, kazi itaendelea vizuri,” amesema Minja.
Aidha, amesema kamati itaendelea kufuatilia kwa karibu utekelezaji wa mradi huo ili kuhakikisha makubaliano yote yaliyowekwa yanatekelezwa kwa wakati na kwa ufanisi.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa DUWASA, Mhandisi Aron Joseph, amesema ziara ya kamati hiyo imelenga kukagua mradi wa kuboresha mtandao wa maji taka katika maeneo ya Area C na Area D.
Ameeleza kuwa mradi huo unahusisha kubadilisha mabomba ya zamani ya zege na kuweka mabomba ya plastiki, ambapo unatekelezwa kwa gharama ya shilingi bilioni 4.9.
Mhandisi Joseph amesema kamati imejionea changamoto zilizokuwepo pamoja na mafanikio yaliyopatikana hadi sasa, na kutoa maelekezo yatakayosaidia kuharakisha utekelezaji wake.
“Mradi huu unalenga kuhudumia takribani kaya 2,700, hivyo ni muhimu ukakamilika kwa wakati ili wananchi wanufaike,” amesema.
Ameongeza kuwa DUWASA imepokea maelekezo ya kamati hiyo na ipo tayari kuyafanyia kazi mara moja ili kuhakikisha mradi unakamilika kwa wakati na kuleta tija kwa wananchi.
Ameishukuru kamati ya bunge kwa ziara yao na kusisitiza kuwa ushirikiano uliopo utaongeza ufanisi katika utekelezaji wa miradi ya maji nchini.





No comments:
Post a Comment