PBPA YAAGIZWA KUHARAKISHA UPOKEAJI NA USAZAMBAZAJI WA MAFUTA NCHINI - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Thursday, March 26, 2026

PBPA YAAGIZWA KUHARAKISHA UPOKEAJI NA USAZAMBAZAJI WA MAFUTA NCHINI


Na Mwandishi Wetu - Dar es Salaam


Waziri wa Nishati, Mhe. Deogratius John Ndejembi ameutaka Wakala wa Uagizaji Mafuta kwa Pamoja (PBPA) kuhakikisha kuwa maghala yote makubwa ya usambazaji wa mafuta yanapata bidhaa hiyo kwa wakati, ili kuimarisha upatikanaji wake nchini.

Hayo yamesemwa leo Machi 26, 2026 jijini Dar es Salaam wakati wa kikao chake na viongozi wa PBPA, Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) na kampuni ya TIPER kwa lengo la kujadili hali ya upokeaji wa mafuta yanayoingia nchini.

Akizungumza katika kikao hicho, Mhe. Ndejembi ameielekeza PBPA kuweka mfumo madhubuti wa upangaji wa ratiba ya ushushaji wa mafuta (sequencing) ili kuhakikisha maghala yote makubwa yanayohusika na usambazaji yanapata mafuta kwa usawa na kwa wakati.

Amesema hatua hiyo itasaidia kupunguza changamoto za upatikanaji wa mafuta katika maeneo mbalimbali ya nchi.

Aidha, ameeleza kuwa Serikali imekubaliana kuharakisha ushushaji wa meli za mafuta zinazoingia nchini, hususan kwa ajili ya matumizi ya ndani, ili kuhakikisha upatikanaji wa mafuta unaendelea kuwa wa uhakika na salama.

Ameongeza kuwa Serikali imefanya mazungumzo na Tanzania International Petroleum Reserves Limited (TIPER), na kuelekeza kuwepo kwa utaratibu mzuri wa kupanga ushushaji wa mafuta ili wasambazaji wote wapate huduma kwa usawa.

Waziri Ndejembi amewaasa Watanzania kutokuwa na taharuki kuhusu upatikanaji wa mafuta, akisisitiza kuwa nchi ina akiba ya kutosha.

Vilevile, Mhe. Ndejembi, ameitaka EWURA kuhakikisha kuwa mafuta yote yanayotoka kwenye maghala yanafika kwa walengwa na kutumika ipasavyo, huku vituo vya mafuta vikihimizwa kuuza bidhaa kulingana na mahitaji halisi ya soko.

Kikao hicho pia kilihudhuriwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati anayeshughulikia Mafuta na Gesi Asilia, Dkt. James Mataragio, Mtendaji Mkuu wa PBPA, Bw. Erasto Simon, Mkurugenzi Mkuu wa EWURA, Dkt. James Andilile pamoja na Mkurugenzi Mtendaji wa TIPER, Bw. Mohamed Mohamed na wataalam mbalimbali wa sekta ya mafuta.

No comments:

Post a Comment