Kamati ya kudumu ya Bunge ya Maji na Mazingira imejadili na kuidhinisha Randama ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maji kwa mwaka
2026/27.
Randama imejadiliwa na wajumbe wa kamati hiyo ikiongozwa na Mwenyekiti wa Kamati Mhe. Jackson Kiswaga (Mb) Bungeni Jijini Dodoma.
Mkurugenzi Msaidizi wa Mipango na Bajeti wa Wizara ya Maji Bw. Tedy Mwaijumba kwa niaba ya Waziri wa Maji amefanya wasilisho la Randama.
Randama imeainisha Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maji kwa Mwaka 2026/2027, pia vipaumbele ikiwemo kuendelea na utekelezaji wa miradi ya maji ya vijiji 867, mabwawa 35 na Miradi 220 ya maji mijini, kuendelea kutekeleza mradi wa kimkakati wa Mpango wa Mtandao wa Taifa wa usambazaji maji (Gridi ya Maji ya Taifa), Matumizi ya Dira janja, kuimarisha usimamizi na uendelezaji wa rasilimali za maji, kuimarisha uendelevu wa huduma za maji na uhimilivu wa mabadiliko ya tabianchi, kupunguza upotevu wa maji, kuendeleza vyanzo mbadala vya fedha ya utekelezaji wa miradi ya maji, kuimarisha Taasisi zilizo chini ya Wizara ya Maji na kuimarisha mfumo wa uratibu wa utekelezaji wa miradi ya maji.
Kuidhinishwa kwa Randama hiyo na Kamati ya Maji na Mazingira kunatoa fursa kwa Wizara ya Maji kuandaa Hotuba ya Bajeti ya 2026/2027 ili kuwasilishwa katika bunge la Bajeti.
Waziri wa Maji Mhe. Jumaa Aweso (Mb) amemshukuru Mwenyekiti wa kamati hiyo Mhe. Jackson Kiswaga (Mb) na Wajumbe wote wa kamati kwa kujadili na kuidhinisha randama hiyo na kuahidi kuzingatia maoni ya kamati katika hotuba ya bajeti.





No comments:
Post a Comment