RAIS DKT. MWINYI AKUTANA NA KAIMU BALOZI WA MAREKANI, AZUNGUMZIA USHIRIKIANO NA FURSA ZA UWEKEZAJI ZANZIBAR - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Monday, March 23, 2026

RAIS DKT. MWINYI AKUTANA NA KAIMU BALOZI WA MAREKANI, AZUNGUMZIA USHIRIKIANO NA FURSA ZA UWEKEZAJI ZANZIBAR


Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi, amekutana na Kaimu Balozi wa Marekani nchini Tanzania, Balozi Andrew Lentz, kwa mazungumzo yaliyojikita katika kuimarisha maeneo mbalimbali ya ushirikiano kati ya Zanzibar na Marekani.

Mazungumzo hayo yamefanyika leo, tarehe 23 Machi 2026, Ikulu, Zanzibar.

Katika mazungumzo hayo, Dkt. Mwinyi amesema ujenzi unaoendelea wa mradi wa Bandari Jumuishi ya Mangapwani unatarajiwa kuondoa changamoto zilizopo na kuongeza kasi ya ukuaji wa uchumi wa Zanzibar kutokana na uwekezaji mkubwa unaoendelea kufanyika.

Amefafanua kuwa mradi huo unajumuisha mitambo ya kuzalisha umeme wa megawati 200, matangi ya hifadhi ya mafuta, pamoja na bandari yenye uwezo wa kuhudumia meli kubwa zaidi, hatua itakayosaidia kupunguza msongamano katika Bandari ya Malindi.

Halikadhalika, Rais Dkt. Mwinyi ameihakikishia Marekani kuendeleza ushirikiano katika nyanja mbalimbali na kuishukuru kwa mchango wake kwa Tanzania, ikiwemo Zanzibar.

Amesisitiza kuwa bado zipo fursa nyingi kwa makampuni na wawekezaji kutoka Marekani kuwekeza nchini.

Kwa upande wake, Kaimu Balozi wa Marekani nchini Tanzania, Balozi Andrew Lentz, amepongeza hatua ya maendeleo inayofikiwa Zanzibar, hususan katika ujenzi wa miundombinu, akieleza kuwa ni msingi muhimu katika kuvutia uwekezaji, kukuza uchumi na kuboresha ustawi wa wananchi.

Vilevile, ameahidi kuwa Marekani itaendelea kupanua maeneo ya ushirikiano na Zanzibar, hususan katika sekta za afya, mabadiliko ya tabianchi, biashara na uwekezaji.




No comments:

Post a Comment