USHIRIKI WA WATANZANIA KATIKA SEKTA YA MADINI WAONGEZWA KUPITIA HUDUMA ZA KISHERIA - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Monday, March 23, 2026

USHIRIKI WA WATANZANIA KATIKA SEKTA YA MADINI WAONGEZWA KUPITIA HUDUMA ZA KISHERIA


Na Mwandishi Wetu - Dodoma.


Serikali kupitia Tume ya Madini imeendelea kusisitiza umuhimu wa utekelezaji madhubuti wa sheria na kanuni katika sekta ya madini, ikiwa ni sehemu ya mkakati wa kuhakikisha rasilimali za taifa zinawanufaisha Watanzania na kulinda maslahi mapana ya nchi.

Akizungumza jijini Dodoma katika kikao kazi kilichowakutanisha wawakilishi wa mawakili kutoka Wizara ya Katiba na Sheria, Ofisi ya Mwasheria Mkuu wa Serikali pamoja na viongozi kutoka Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) na taasisi ya Breakthrough Attorneys, Mkurugenzi wa Ukaguzi na Biashara ya Madini, CPA Venance Kasiki, amesema wanasheria na kampuni za sheria ni wadau muhimu katika kuimarisha ufuataji wa sheria na utatuzi wa migogoro katika sekta hiyo.

Amesema uwepo wa ushauri bora wa kisheria unachangia kuongeza ufanisi wa shughuli za uchimbaji, hususan kwa wamiliki wa leseni, wakandarasi na watoa huduma migodini, hivyo kuchochea ukuaji endelevu wa sekta ya madini.

CPA Kasiki amefafanua kuwa kikao hicho kimeandaliwa mahsusi kujenga uelewa wa pamoja kuhusu utekelezaji wa Kanuni ya 13A ya Kanuni za Ushirikishwaji wa Watanzania katika nyanja ya huduma za kisheria, akisisitiza umuhimu wa wadau hao kuzingatia weledi, uadilifu, uwazi na gharama nafuu katika utoaji wa huduma zao.

“Ni muhimu kwa kampuni za sheria na wanasheria binafsi kuhakikisha wanatoa huduma zenye viwango vya juu vya taaluma, zitakazochochea uwekezaji na kulinda maslahi ya Taifa,” amesema CPA Kasiki.

Aidha, amewataka wanasheria wa ndani kujenga uwezo wa kitaaluma ili waweze kushindana katika miradi mikubwa ya kimkakati, hususan katika kukabiliana na changamoto ya kuoanisha mikataba ya kimataifa na sheria za ndani.

Kwa upande mwingine, maboresho ya Sheria ya Madini, Sura ya 123 pamoja na kanuni zake, yameendelea kuweka mkazo katika kuongeza ushiriki wa Watanzania kupitia utoaji wa kipaumbele kwa bidhaa na huduma za ndani, ikiwemo huduma za kisheria.

Amesema utekelezaji wa Kanuni za Ushirikishwaji wa Watanzania za mwaka 2018 umeleta mafanikio makubwa, yakiwemo ongezeko la ajira, kukuza matumizi ya bidhaa na huduma za ndani, uhamishaji wa teknolojia pamoja na kuongeza uelewa wa wananchi kuhusu nafasi yao katika sekta ya madini.

CPA Kasiki amebainisha kuwa wanasheria wana jukumu la msingi katika kuhakikisha mafanikio hayo yanaendelea kudumishwa, ikiwa ni pamoja na kutoa ushauri wa kisheria, kusimamia mikataba ya ubia, kuhakikisha kipaumbele kinatolewa kwa Watanzania katika ajira na huduma, pamoja na kushiriki kikamilifu katika utatuzi wa migogoro.

Kikao kazi hicho kimejadili kwa kina uwezo, mchango na mafanikio ya kampuni za sheria zinazomilikiwa kwa asilimia 100 na Watanzania, pamoja na kubaini changamoto zilizopo na kupendekeza mikakati ya kuboresha ushiriki wao katika sekta ya madini.

No comments:

Post a Comment