RAIS SAMIA AIPONGEZA NA KUIELEKEZA PPRA, NeST YAOKOA ZAIDI YA SH. BILIONI 13.5 - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Tuesday, March 31, 2026

RAIS SAMIA AIPONGEZA NA KUIELEKEZA PPRA, NeST YAOKOA ZAIDI YA SH. BILIONI 13.5


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, ameipongeza Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA) kwa kusimamia kwa ufanisi Mfumo wa NeST, unaoimarisha uwazi na uwajibikaji katika michakato ya ununuzi wa umma.

Akizungumza baada ya kupokea Taarifa ya Utendaji Kazi ya Mamlaka hiyo kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025, tarehe 30 Machi 2026, Ikulu, Dar es Salaam, Rais Samia amewataka viongozi wa taasisi zote za umma kuhakikisha wanasimamia kikamilifu taratibu za ununuzi wa umma ili kulinda fedha za wananchi na kuhakikisha zinatumika kwa manufaa yaliyokusudiwa.

Aidha, Rais Samia ameielekeza PPRA kuwataja hadharani viongozi na taasisi zinazofanya vibaya ili kuongeza uwajibikaji, ufanisi na uadilifu katika utendaji wa taasisi za umma.

“Vilevile, nikuelekeze Mkurugenzi Mkuu wa PPRA, ili tuweze kusimamia vizuri taasisi zetu kuna kitu kinaitwa ‘Name and Shame’. Hivyo, katika ripoti yako ya mwaka ujao, tutajie wanaofanya vibaya zaidi na wanaofanya vizuri zaidi.
Hii itawatia motisha wale wanaofanya vibaya kujirekebisha,” amesema Rais Samia.

Katika hatua nyingine, Rais ameziagiza Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, kwa kushirikiana na Wizara ya Fedha pamoja na Ofisi ya Rais - Menejimenti ya Utumishi wa Umma, kuendelea kusimamia kikamilifu zoezi la kuunganisha mifumo mingine ya Serikali na Mfumo wa NeST.

Maelekezo hayo yamekuja kufuatia taarifa ya Mkurugenzi Mkuu wa PPRA, Bw. Dennis Simba, kuwa Mfumo wa NeST tayari umeunganishwa na mifumo 21 ya Serikali, huku jitihada za kuunganisha mifumo mingine zikiendelea.

Awali, akiwasilisha taarifa ya Mamlaka hiyo, Bw. Simba alieleza kuwa matumizi ya Mfumo wa NeST yamewezesha kuokoa zaidi ya Shilingi Bilioni 13.5 kutokana na kupunguza matumizi ya karatasi na toner.

 Aliongeza kuwa PPRA inaendelea kufanya tathmini kubaini kiasi kinachookolewa na wazabuni kutokana na kupungua kwa gharama za safari, uchapishaji na uwasilishaji wa zabuni.
Aidha, Mamlaka ilifanikiwa kuokoa zaidi ya Shilingi Milioni 634.1 kupitia uchunguzi maalum uliofanyika katika taasisi nunuzi 16.

“Tumechukua hatua kwa wazabuni 34 kwa kushindwa kutekeleza mikataba, kughushi nyaraka, kutozingatia tamko la dhamana la zabuni na dhamana la utekelezaji wa mikataba,” alisema Bw. Simba.

No comments:

Post a Comment