Vijana wa Kijiji cha Holili, kilichopo kata ya Holili, Wilaya ya Rombo Mkoani Kilimanjaro, wameaswa kushirikiana na Jeshi la Polisi katika kutimiza kwa vitendo dhima ya Polisi jamii ikiwa ni kuzuia, kubaini na kutanzua uhalifu katika maeneo ya Kijiji hicho ambapo ni mpaka kati ya Nchi ya Tanzania na Kenya.
Akizungumza na Vijana hao Machi 30, 2026 Mkuu wa ushirikishwaji jamii kutoka Kikosi cha Kuzuia Wizi wa Mifugo Nchini (STPU) Mrakibu Mwandamizi wa Polisi SSP Juma Bonza, alisema kuwa katika kuzuia uhalifu ambao umekuwa ukijitokeza katika maeneo ya mipakani ikiwa ni pamoja na usafirishaji wa mifugo bila vibali ni vyema Vijana hao wakashirikiana na Polisi Kata katika kutimiza dhima ya Polisi jamii kwa vitendo, ikiwa ni pamoja na kutoa taarifa mara baada ya kuona viashiria vya uhalifu katika eneo hilo.
Aidha, alitoa wito kwa vijana hao kuepukana na matumizi ya madawa ya kulevya ambayo hupelekea kuathiri nguvu kazi ya taifa badala yake wajikite katika kuchangamkia fursa mbalimbali za kujiingizia kipato ambazo zinapatikana katika eneo hilo la mpakani.
Katika hatua nyingine mkuu huyo wa ushirikishwaji jamii aliwakumbusha vijana hao madhara ya kujichukulia sheria mkononi huku akisema kuwa kwa kufanya hivyo hakupelekei kutokomeza uhalifu badala yake wawatumie viongozi wa Serikali za mitaa wa eneo hilo pamoja na Polisi Kata katika kufuata sheria na taratibu za kuzuia uhalifu na wahalifu katika maeneo yao.





No comments:
Post a Comment