SERIKALI YAIMARISHA HUDUMA KWA WENYE ULEMAVU KUPITIA MFUMO WA PD-MIS - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Thursday, March 26, 2026

SERIKALI YAIMARISHA HUDUMA KWA WENYE ULEMAVU KUPITIA MFUMO WA PD-MIS



Na Mwandishi Wetu, Ruvuma


Serikali imeendelea kuchukua hatua madhubuti za kuboresha huduma kwa watu wenye ulemavu kwa kuwajengea uwezo watendaji wake katika matumizi ya mfumo wa kielektroniki wa ukusanyaji na usimamizi wa taarifa za watu wenye ulemavu (PD-MIS), hatua inayolenga kupata takwimu sahihi kuanzia ngazi ya kaya hadi mkoa.

Mafunzo hayo yamehusisha Maafisa Tehama na Maafisa Ustawi wa Jamii kutoka Mikoa ya Ruvuma, Mtwara, Lindi na Njombe, yakifanyika mkoani Ruvuma tarehe 26 Machi 2026, kwa lengo la kuwawezesha washiriki kutambua na kusimamia matumizi ya mfumo huo katika maeneo yao ya kazi.

Akizungumza wakati wa mafunzo hayo, Afisa kutoka Kitengo cha Huduma kwa Watu Wenye Ulemavu, Ofisi ya Waziri Mkuu – Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu, Bw. Jackob Mwinula, alisema kuwa uwezeshaji huo ni muhimu katika kuhakikisha watendaji wanakuwa na uelewa wa kutosha wa mfumo huo na kuwafikia wananchi kwa ufanisi zaidi.

“Baada ya mafunzo haya, tunatarajia kuona watu wenye ulemavu wakisajiliwa, kupata namba za utambulisho na hivyo kuwezeshwa kufikia huduma mbalimbali za kijamii pamoja na kuunganishwa na mifumo mingine ya Serikali,” alisema Bw. Mwinula.

Aliongeza kuwa zoezi la usajili ni endelevu na litahusisha maafisa kuwafikia walengwa moja kwa moja katika maeneo wanayoishi ili kuhakikisha hakuna anayebaki nyuma.

Kwa upande wake, Bi. Suzana Mayengo, mwezeshaji kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu, alisema mafunzo hayo pia yanalenga kuwajengea watendaji uwezo wa kutambua aina mbalimbali za ulemavu na namna ya kushirikisha kundi hilo katika mipango ya maendeleo ili kuhakikisha ushirikishwaji jumuishi na unaozingatia mahitaji yao.

Aidha, upatikanaji wa taarifa sahihi utaiwezesha Serikali kutekeleza kikamilifu Mkataba wa Kimataifa wa Haki za Watu Wenye Ulemavu wa mwaka 2006 unaosisitiza kauli mbiu ya “Nothing About Us Without Us”, inayolenga ushirikishwaji wa moja kwa moja wa kundi hilo katika maamuzi yanayowahusu.

Naye Mchambuzi wa Mifumo kutoka Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA), Bw. Antony Nchimbi, alieleza kuwa mfumo wa (PD-MIS) umesanifiwa kwa ushirikiano kati ya e-GA na Ofisi ya Waziri Mkuu, na umeunganishwa na mifumo mingine 11 ya Serikali ili kurahisisha upatikanaji na ubadilishanaji wa taarifa.

Alibainisha kuwa mfumo huo una uwezo wa kuwasiliana na mifumo muhimu ikiwemo wa wanafunzi (SIS) kutoka TAMISEMI, mfumo wa afya (GoTHOMIS), mfumo wa mikopo (Wezesha) na Mfumo wa Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu (HESLB), hatua itakayosaidia kuthibitisha na kuboresha huduma kwa watu wenye ulemavu nchini.






No comments:

Post a Comment