TANZANIA NA IRELAND KUPANUA UFADHILI WA MASOMO YA TEKNOLOJIA - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Thursday, March 26, 2026

TANZANIA NA IRELAND KUPANUA UFADHILI WA MASOMO YA TEKNOLOJIA



Na Francis Peter,OKULY BLOG - Dar es Salaam


Serikali ya Tanzania na Ireland zimesaini hati ya makubaliano (MoU) yenye lengo la kuendeleza ushirikiano katika utoaji wa ufadhili wa masomo kwa wanafunzi wa Kitanzania wanaofanya vizuri katika masomo ya sayansi kupitia programu ya Samia Scholarship Extended DS/AI.

Kupitia programu hiyo, wanafunzi bora wa kidato cha sita wanapata fursa ya kusoma Shahada ya Kwanza katika masomo ya sayansi ya data, akili unde (AI) na ubunifu katika chuo Kikuu cha Limerick nchini Ireland.

Akizungumza jijini Dar es Salaam, leo Machi 26, 2026, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda amesema makubaliano hayo yanakwenda kufungua fursa zaidi akibainisha huo ni utekelezaji wa maelekezo ya Rais Samia Suluhu Hassan, ya kupanua fursa za elimu ya juu katika maeneo ya teknolojia na ubunifu.

Profesa Mkenda amesema kadri fursa zinavyopatikana ndipo watapanua wigo wa ufadhili kwa wanafunzi, akisisitiza watakaonufaika na mpango huo ni wale tu wenye ufaulu wa juu katika masomo ya sayansi ili kutoa nafasi sawa kwa vijana kutoka makundi mbalimbali ya kijamii.

"Kwa mwaka huu, wanafunzi 50 wanatarajiwa kunufaika na ufadhili huo, huku idadi ikitarajiwa kuongezeka kadiri fursa zinavyozidi kupanuliwa," amesema.

Naye Makamu wa rais wa Chuo Kikuu cha Limerick anayeshughulikia masuala ya kimataifa, Profesa Colin Fitzpatrick, amesema wanafunzi watakaokwenda kusoma nchini Ireland watapata uzoefu wa kimataifa kupitia mafunzo kwa vitendo na fursa za ajira katika kampuni kubwa za nchini humo zinazoshirikiana na chuo hicho.

Balozi wa Ireland nchini Tanzania, Nicola Brennan amesema ushirikiano huo unalenga kuimarisha mapinduzi ya kiuchumi kupitia elimu na ubunifu.

No comments:

Post a Comment