
Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar (Mb), akizungumza katika Warsha ya Shirika la Bima ya Maendeleo ya Biashara na Uwekezaji Afrika (ATIDI) na wadau wa Maendeleo kuhusu “Kuimarisha Mazingira ya Biashara na Uwekezaji Tanzania” iliyofanyika hoteli ya Hyatt Regency jijini Dar es Salaam, ambapo alilisifu shirika hilo kwa mchango wake mkubwa katika kutoa huduma za kupunguza hatari za uwekezaji (de-risking), hatua inayowapa wawekezaji na taasisi za kifedha ujasiri wa kushiriki katika miradi mikubwa barani Afrika.

MKurugenzi Mkuu wa Shirika la Bima ya Maendeleo ya Biashara na Uwekezaji Afrika (ATIDI), Bw. Manuel Moses, akimkaribisha Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar (Mb) (hayupo pichani), kuhutubia katika Warsha ya Shirika la Bima ya Maendeleo ya Biashara na Uwekezaji Afrika (ATIDI) na wadau wa Maendeleo kuhusu “Kuimarisha Mazingira ya Biashara na Uwekezaji Tanzania” iliyofanyika hoteli ya Hyatt Regency jijini Dar es Salaam.

Mwenyekiti wa Bodi ya Taasisi ya Bima ya Maendeleo ya Biashara na Uwekezaji Afrika (ATIDI), Prof. Kelly Kingsly, akizungumza wakati wa Warsha ya Shirika la Bima ya Maendeleo ya Biashara na Uwekezaji Afrika (ATIDI) na wadau wa Maendeleo kuhusu “Kuimarisha Mazingira ya Biashara na Uwekezaji Tanzania” iliyofanyika hoteli ya Hyatt Regency jijini Dar es Salaam.

Meza Kuu ikiongozwa na Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar (Mb) (Katikati), wakiwa katika picha ya pamoja katika Warsha ya Shirika la Bima ya Maendeleo ya Biashara na Uwekezaji Afrika (ATIDI) na wadau wa Maendeleo kuhusu “Kuimarisha Mazingira ya Biashara na Uwekezaji Tanzania” iliyofanyika hoteli ya Hyatt Regency jijini Dar es Salaam.

Meza Kuu ikiongozwa na Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar (Mb) (Katikati), wakiwa katika picha ya pamoja na wadau mbalimbali wa maendeleo, wakati wa Warsha ya Shirika la Bima ya Maendeleo ya Biashara na Uwekezaji Afrika (ATIDI) na wadau hao kuhusu “Kuimarisha Mazingira ya Biashara na Uwekezaji Tanzania” iliyofanyika hoteli ya Hyatt Regency jijini Dar es Salaam.
(Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, WF, Dar es Salaam)
Na Benny Mwaipaja, Dar es Salaam
Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar (Mb) amesema kuwa Tanzania itaendelea kuimarisha zaidi ushirikiano na Shirika la Bima ya Maendeleo ya Biashara na Uwekezaji Afrika (ATIDI) katika juhudi za kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji nchini, sambamba na kuvutia mitaji zaidi ya sekta binafsi kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mikubwa ya maendeleo.
Akizungumza jijini Dar es Salaam katika Warsha ya ATIDI kuhusu “Kuimarisha Mazingira ya Biashara na Uwekezaji Tanzania” iliyofanyika hoteli ya Hyatt Regency, Mhe. Balozi Omar alilisifu shirika hilo kwa mchango wake mkubwa katika kutoa huduma za kupunguza hatari za uwekezaji (de-risking), hatua inayowapa wawekezaji na taasisi za kifedha ujasiri wa kushiriki katika miradi mikubwa barani Afrika.
“Tanzania inajivunia kuwa si tu mwanachama, bali pia ni miongoni mwa waanzilishi wa ATIDI, shirika lililoundwa kutoa suluhisho za Kiafrika kwa changamoto za Kiafrika,” alisema Balozi Omar.
Alisema licha ya Bara la Afrika kuwa na fursa kubwa za uwekezaji, bado limekuwa likikabiliwa na mtazamo hasi kuhusu hatari za mikopo na uwekezaji jambo lililosababisha haja ya kuanzishwa kwa ATIDI.
Alibainisha kwamba huduma za bima na dhamana zinazotolewa na ATIDI zimeanza kuongeza imani ya wawekezaji, hivyo kuchochea ufadhili wa miradi muhimu katika sekta za miundombinu, viwanda, na nishati.
Mhe. Balozi Omar alisema kuwa Tanzania, ni miongoni mwa wanaonufaika zaidi na huduma za ATIDI, ikinufaika na miradi yenye thamani ya dola za Marekani bilioni 7.8, ikiwemo sehemu ya Mradi wa Reli ya Kisasa (SGR).
Alisisitiza kuwa ushirikiano wenye tija kati ya Tanzania na ATIDI unakwenda sambamba na utekelezaji wa Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050, inayolenga kubadilisha kabisa muundo wa uchumi kupitia mageuzi ya viwanda, uboreshaji wa miundombinu, na uwekezaji unaoongozwa na sekta binafsi.
Dira hiyo inalenga kuongeza Pato la Taifa (GDP) mara kumi na kuifikisha Tanzania katika hadhi ya uchumi wa kipato cha juu, licha ya ongezeko la watu na kwamba Ili kufanikisha hilo, kunahitajika uratibu mkubwa zaidi katika sekta ya fedha, ikiwemo taasisi za kupunguza hatari kama ATIDI.
“Afrika inapaa. Ni wakati wa kuzichangamkia fursa, si tu ndani ya mipaka yetu bali pia katika ukanda mzima na bara lote la Afrika,” alisema Mhe. Balozi Omar.
Aliahidi kuwa serikali itaendelea kushirikiana kwa karibu na ATIDI na wadau wengine katika kuunda mfumo wa kifedha wenye ufanisi zaidi unaoendana na ukuaji wa uchumi unaoongozwa na sekta binafsi.
Pia alisema serikali imejikita katika kuhakikisha mazingira rafiki ya biashara pamoja na sera za kodi zinazounga mkono ukuaji wa uchumi.
Kwa upande wake, MKurugenzi Mkuu wa Shirika la Bima ya Maendeleo ya Biashara na Uwekezaji Afrika (ATIDI), Bw. Manuel Moses amesema kuwa Taasisi yake itaendelea kushirikiana kwa karibu na Serikali ya Tanzania katika juhudi za kuimarisha mazingira ya biashara na uwekezaji, huku akihamasisha mitaji zaidi kuingia nchini kupitia miradi mikubwa ya maendeleo yenye tija kwa uchumi wa taifa.
Alisema kuwa Afrika ina fursa nyingi za uwekezaji na biashara, lakini changamoto imekuwa ni ukosefu wa mifumo na vyombo imara vya kupunguza hatari zinazowakabili wawekezaji.
Bw. Moses alieleza kuwa tangu kuanzishwa kwake mwaka 2001, ATIDI imekua na kuwa mtoa huduma mkubwa zaidi wa bima ya biashara na uwekezaji barani Afrika, ikiwa tayari imesaidia uwekezaji na biashara za mipakani zenye thamani ya zaidi ya dola bilioni 93 katika nchi mbalimbali za bara hilo.
“Kwa upande wa Tanzania pekee, shirika limekuwa na mchango mkubwa katika miradi ya kimkakati yenye thamani ya zaidi ya dola bilioni 7.8, ikiwemo miradi ya miundombinu ya viwanja vya ndege, reli, barabara, madaraja, mawasiliano, makazi ya gharama nafuu, na miradi kadhaa ya nishati inayoratibiwa na TANESCO na Wakala wa Nishati Vijijini (REA). ATIDI pia limekuwa likiunga mkono taasisi za kifedha, benki za ndani na kampuni binafsi, zikiwemo biashara ndogo na za kati (SMEs)”alisema Bw. Moses
Vilevile, shirika hilo limefadhili miradi mikubwa ya kijamii ikiwemo Mradi wa Uthabiti wa Gridi ya Taifa wenye thamani ya dola milioni 200, na Mradi wa Usafi wa Mazingira ulio na thamani ya dola milioni 150 katika mikoa kadhaa ya Tanzania.
ATIDI limesema miradi hiyo imechangia kuimarisha miundombinu ya msingi, kuongeza upatikanaji wa huduma muhimu, na kusaidia kufanikisha mageuzi ya kiuchumi na kijamii nchini.
ATIDI (zamani ikiitwa African Trade Insurance Agency – ATI) ni shirika la kikanda linalotoa huduma za bima za uwekezaji, dhamana za biashara, na usaidizi wa kifedha ili kupunguza hatari kwa wawekezaji barani Afrika. Tanzania ni miongoni mwa wanachama waanzilishi na imenufaika sana kupitia huduma zake ambazo zimewezesha utekelezaji wa miradi mikubwa ya kitaifa ya maendeleo.

No comments:
Post a Comment