
Mradi wa kuimarisha jamii na mifumo ikolojia katika kuhimili mabadiliko ya tabianchi ukanda wa misitu ya miombo umepanga kutumia Shilingi Bilioni 2.6 kwa mwaka 2025/26-2026/27 kwa ajili ya utekelezaji wa shughuli za mradi huo.
Akifungua kikao cha kamati tendaji ya Mradi huo Machi 26, 2026 Jijini Dodoma, Naibu Katibu Mkuu (Mazingira) Ofisi ya Makamu wa Rais, Mhe. Balozi Baraka Luvanda amesema mradi huo unatekelezwa katika misitu ya miombo Tanzania Bara na Maeneo Kame Zanzibar.
Amesema mradi huo unatekelezwa na Ofisi ya Makamu wa Rais kwa kushirikiana na Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais-Zanzibar, Wizara ya Kilimo, Umwagiliaji, Maliasili na Mifugo-Zanzibari, na Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS).
“Mradi huu umekusudia kuboresha na kuimarisha mazingira wezeshi ili kukuza matumizi ya teknolojia za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi katika sekta za kipaumbele hapa nchini amesema Balozi Luvanda.
Mhe. Balozi Luvanda amebainisha kuwa mradi huo pia utaongeza mnyororo wa thamani ya mazao yasiyokuwa ya misitu, mbogamboga na malisho ya mifugo kwa ukanda wa maeneo ya miombo kwa Tanzania Bara na upande wa Zanzibar.
Amesema dhamira ya Ofisi ya Makamu wa Rais ni kuhakikisha inaongeza furs ana wigo wa upatikanaji wa miradi ya kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi nchini kujenga uwezo kwa jamii zenye changamoto ya rasilimali fedha na uelewa mdogo wa mbinu za uzalishaji wa mazao.
Kwa upande wake Mratibu wa Mradi, Bw. James Chuyi amesema mradi huo unatekelezwa katika Mikoa saba iliyopo katika Halmashauri saba nchini kutoka upande wa Tanzania Bara na Zanzibar.
Ameitaja Mikoa hiyo kuwa ni Tabora (Sikonge), Rukwa (Nkasi), Katavi (Mpanda), Kaskazini Unguja (Kaskazini B), Kusini Unguja (Wilaya ya Kusini), Kaskazini Pemba (Micheweni) na Mkoa wa Kusini Pemba (Chakechake).
Mradi wa kuimarisha jamii na mifumo ikolojia katika kuhimili mabadiliko ya tabianchi ukanda wa misitu ya miombo unatekelezwa katika kipindi cha miaka mitano kuanzia mwaka 2025-2029 na unafadhiliwa wa Mfuko wa Dunia wa Mazingira (GEF) kupitia usimamizi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Chakula na Kilimo (FAO).





No comments:
Post a Comment