
Serikali ya Tanzania imewakaribisha wawekezaji wa kimkakati kutoka duniani kote kuja kuwekeza katika sekta ya nishati safi ili kuchochea ukuaji wa uchumi na kusadia jitihada za Serikali za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.
Mwaliko huo umetolewa na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Ngw'aru Maghembe alipozungumza kwenye Jopo la Majadilino kuhusu mada isemayo “Kupanga Maendeleo kwa Ubunifu: Ili Kujenga Ukuaji wa Dunia wa Kesho” wakati wa Mkutano wa Jukwaa la Raisina 2026 unaofanyika jijini New Delhi, India kuanzia Machi 5 hadi 7, 2026.
Wakati wa majadiliano hayo ambayo yalijikita kwenye umuhimu wa usalama wa nishati kama nguzo muhimu ya maendeleo endelevu kwa nchi mbalimbali duniani, Mhe. Maghembe alisema, Tanzania chini ya uongozi imara wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, imeendelea kuimarisha usalama wa nishati kwa kuwekeza katika miradi mikubwa ya kuzalisha umeme ukiwemo ule wa Julius Nyerere-JNHPP wenye uwezo wa kuzalisha Megawati 2,115 pamoja na miradi mingine ya gesi asilia na vyanzo mbadala.
Aliongeza kusema, Serikali ya Tanzania katika kutekeleza agenda ya matumizi ya nishati safi ya kupikia ambapo mwaka 2024 ilizindua Mkakati wa Taifa wa matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia wa miaka 10. Mkakati huu pamoja na mambo mengine unalenga kuhamasisha matumizi ya nishati safi ili kupunguza matumizi ya mkaa na kuni, lengo likiwa kufikia asilimia 80 ya matumizi ya nishati hiyo kwa kaya ifikapo mwaka 2030.
“Ni kutokana na jitihada hizo, Tanzania inawakaribisha wawekezaji kutoka duniani kote kuja kuwekeza kwenye miradi mbalimbali ya kuzalisha nishati mbadala, usambazaji wa gesi asilia na miradi mingine ya nishati safi, kupitia utaratibu wa ubia kati ya sekta ya umma na sekta binafsi (PPP)” ili kuendelea kutunza mazingira na kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, alisema Mhe. Dkt. Maghembe.
Aidha, Mhe. Dkt. Maghembe alitumia fursa hiyo kutoa wito kwa nchi zilizoendelea kutimiza ahadi zao kwa nchi zinazoendelea wa kuziwezesha kupunguza athari za mabadiliko ya tabianchi.












No comments:
Post a Comment