Wanufaika wa Mikopo ya Asilimia 10 Morogoro Watakiwa Kuitumia kwa Maendeleo - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Saturday, March 7, 2026

Wanufaika wa Mikopo ya Asilimia 10 Morogoro Watakiwa Kuitumia kwa Maendeleo


Wanufaika wa mikopo ya asilimia 10 inayotolewa na Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro wametakiwa kuhakikisha wanatumia fedha hizo kwa malengo yaliyokusudiwa ili ziweze kuleta tija katika maisha yao na kuchochea maendeleo ya kiuchumi kwa jamii

Wito huo umetolewa na Mstahiki Meya wa Manispaa ya Morogoro, Khalid Matengo, wakati wa hafla ya utoaji wa mikopo ya asilimia 10 ya mapato ya ndani ya manispaa hiyo kwa makundi ya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu. Amesema kuwa mikopo hiyo ni fursa muhimu kwa wananchi kujikwamua kiuchumi, hivyo ni lazima itumike kwa shughuli za uzalishaji na biashara zitakazowawezesha wanufaika kurejesha mikopo kwa wakati na kuinua vipato vyao.


Matengo amesisitiza kuwa matumizi sahihi ya mikopo hiyo yataongeza imani kwa halmashauri kuendelea kutoa mikopo kwa makundi zaidi, huku akiwahimiza wanufaika kuwa waaminifu na kuwajibika katika usimamizi wa fedha wanazopokea.

Akitoa taarifa ya utoaji wa mikopo hiyo, Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro, Emmanuel Mkongo, amesema katika awamu hiyo vikundi 67 vimefanikiwa kunufaika na mikopo hiyo baada ya kukidhi vigezo vilivyowekwa. Hata hivyo amesema vikundi 31 vilishindwa kupata mikopo kutokana na kukosa sifa stahiki pamoja na kubainika kuwepo kwa udanganyifu katika baadhi ya maombi yaliyowasilishwa.

Kwa upande wake Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Morogoro, Josephine Kapoma, amewahimiza wanawake kujitokeza kwa wingi kuunda na kujiunga katika vikundi vinavyotambulika ili waweze kunufaika na mikopo hiyo, akieleza kuwa mpango huo ni nyenzo muhimu ya kuwawezesha wanawake kiuchumi na kuwapa uwezo wa kushiriki kikamilifu katika shughuli za maendeleo.

Naye mmoja wa wanufaika wa mkopo huo, Moses Mbonge, amesema kabla ya kupata mkopo huo alikuwa akipitia changamoto katika ajira za kuajiriwa, lakini baada ya kuupata ameweza kuanzisha shughuli zake za kiuchumi ambazo zimemsaidia kuboresha maisha yake. Amesema mkopo huo umekuwa na tija kubwa kwake na kuwataka vijana wengine kutumia fursa hiyo kubuni na kuendeleza biashara zitakazowaingizia kipato.

Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro inaendelea kutekeleza mpango wa utoaji wa mikopo ya asilimia 10 ya mapato ya ndani kwa lengo la kuwezesha makundi maalum kujikwamua kiuchumi na kuchangia maendeleo ya jamii kwa ujumla.

No comments:

Post a Comment