Na WMJJWM, Morogoro
Watoto 33 waliokuwa wakiishi na kufanya kazi mitaani mkoani Morogoro wameunganishwa na familia zao kufikia Februari 2026.
Afisa Ustawi wa Jamii wa dawati la huduma za ustawi wa jamii katika kituo cha mabasi Msamvu, Pius Marco, amebainisha hayo Machi 25, 2026 mbele ya wawakilishi wa Wizara za kisekta baada ya ziara ya usimamizi Shirikishi katika huduma za Ustawi wa Jamii mkoani humo.
Marco amesema mafanikio hayo yametokana na kampeni endelevu za utoaji elimu kwa jamii inayotolewa na Maafisa Ustawi wa Jamii wa dawati la huduma za Ustawi katika kituo cha mabasi Msamvu, kwa lengo la kuwahamasisha wananchi, hasa madereva wa vyombo vya usafiri, wafanyabiashara sokoni na waendesha bodaboda, kushiriki katika kuwabaini na kuwaokoa watoto wanaoishi mitaani.
Marco ameongeza kwamba watoto hao wakiwemo wasichana 26 na wavulana 7 waliokolewa kutoka mazingira hatarishi ikiwemo kuzurura katika eneo la kituo cha mabasi Msamvu na wengine walifanya kazi hatarishi mitaani wamerejeshwa nyumbani kutokana na ushirikiano wa karibu kati ya Serikali na wadau wa maendeleo.
“Tumefanikiwa kwa sababu ya ushirikiano mzuri wa wadau na mwitikio wa jamii. Watu wengi sasa wanatambua wajibu wao katika kulinda watoto na kutoa taarifa pale wanapowaona katika mazingira hatarishi.” amesema Marco.
Kwa upande wake, Afisa Ustawi wa Jamii kutoka Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum. Timu ya wizara inepongeza juhudi zinazofanywa katika dawati hilo la huduma za jamii kwani linasaidia watoto wanaoishi katika mazingira hatarishi kupata huduma za Ustawi wa Jamii.
Vilevile, Timu ya wizara imesisitiza umuhimu wa kuendelea kutoa elimu kwa wananchi wanaofika katika stendi ya Msamvu ili kuzuia watoto kuingia mitaani na kujihusisha na shughuli zinazoweza kuhatarisha maisha yao.







No comments:
Post a Comment