Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar (Mb), amezindua rasmi Mkutano wa Mapitio ya Pamoja ya Sekta ya Maji (Joint Water Sector Review) na kusisitiza umuhimu wa ushirikiano wa wadau katika kuhakikisha upatikanaji wa maji safi na salama kwa Watanzania wote.
Akizungumza katika mkutano huo uliofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Cate Convention Centre, Morogoro, Mhe. Balozi Omar alisema kuwa sekta ya maji ni mhimili muhimu wa maendeleo ya kijamii na kiuchumi, na hivyo inahitaji uwekezaji endelevu na usimamizi madhubuti wa rasilimali za maji.
Alisema Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imeendelea kuthamini mchango wa sekta hiyo na kushirikiana na wadau mbalimbali katika kufanikisha utekelezaji wa Programu ya Maendeleo ya Sekta ya Maji (WSDP 2006–2026).
Mhe. Balozi Omar alimpongeza Waziri wa Maji, Mheshimiwa Jumaa Hamidu Aweso, pamoja na watendaji wa sekta hiyo kwa mafanikio yaliyopatikana katika kipindi cha miaka 20 ya utekelezaji wa programu hiyo.
Alieleza kuwa upatikanaji wa maji safi mijini umeongezeka kutoka asilimia 74 mwaka 2006 hadi kufikia asilimia 92.5 mwaka 2025, huku vijijini ukiongezeka kutoka asilimia 54 hadi asilimia 85.2, ambapo lengo la vijijini tayari limevukwa.
“Haya ni mafanikio makubwa ya kujivunia, yanayoonesha juhudi za Serikali na wadau wake katika kuboresha huduma za maji nchini,” alisema.Mhe. Balozi Omar.
Pamoja na mafanikio hayo, Mhe. Balozi Omar alibainisha changamoto zilizopo, zikiwemo upungufu wa fedha, athari za mabadiliko ya tabianchi na utekelezaji usioridhisha wa baadhi ya miradi ya maji vijijini kabla ya kuanzishwa kwa Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA).
Alitolea mfano athari za ukame uliopunguza mtiririko wa maji katika Mto Ruvu, uliosababisha changamoto katika upatikanaji wa maji kwa mikoa ya Dar es Salaam na Pwani, na kusisitiza umuhimu wa kuhifadhi vyanzo vya maji na kupanda miti.
Aidha, Mhe. Balozi Omar alieleza kuwa bado vijiji 1,575 havijafikiwa na huduma ya maji, huku Serikali ikiwa imeweka mikakati ya kuhakikisha wananchi wa maeneo hayo wanapata huduma hiyo muhimu.
Alisema kuwa jumla ya shilingi bilioni 883.93, sawa na dola za Marekani milioni 351.04, zilipatikana katika kipindi cha Januari hadi Desemba 2025 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maji na usafi wa mazingira.
Mhe. Balozi Omar aliwataka wadau kuzingatia ubunifu katika utafutaji wa fedha, kuimarisha ushiriki wa sekta binafsi, pamoja na kuweka mkakati wa utekelezaji wa miradi mikubwa ikiwemo Gridi ya Taifa ya Maji ili kuchochea ukuaji wa uchumi.
Aliongeza kuwa mkutano huo ni jukwaa muhimu la kutathmini utekelezaji wa programu ya sekta ya maji na kuandaa mikakati mipya itakayokwenda sambamba na Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.
“Ni muhimu pia kuunganisha nguvu za wadau mbalimbali ili kutekeleza miradi mikubwa yenye tija na huduma ya uhakika kwa wananchi,” alisisitiza.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji, Mhandisi Mwajuma Juma Waziri, amesema Serikali itaendelea kuimarisha sekta ya maji kwa kuweka mikakati madhubuti itakayohakikisha upatikanaji wa maji safi na salama kwa Watanzania wote pamoja na kuchochea maendeleo ya kiuchumi.
Alisema mkutano huo ni sehemu ya maadhimisho ya Wiki ya Maji Duniani, kuelekea kilele cha Siku ya Maji Duniani kinachoadhimishwa Machi 22 kila mwaka, ambapo kaulimbiu ya mwaka huu ni “Maji na Jinsia” ikisisitiza umuhimu wa usawa wa kijinsia katika usimamizi wa rasilimali za maji.
Mhandisi Waziri alisisitiza kuwa maji ni rasilimali muhimu katika maendeleo ya kijamii na kiuchumi, yakichangia katika sekta za afya, kilimo, nishati, viwanda, utalii na usafirishaji, hivyo Serikali inaendelea kuimarisha usimamizi wake ili kuhakikisha uendelevu wake.
Akizungumzia mwelekeo wa baada ya kukamilika kwa Programu ya Maendeleo ya Sekta ya Maji mwaka 2026, Mhandisi Waziri alisema sekta hiyo itajikita katika maeneo muhimu ikiwemo kuhakikisha usalama wa maji, kuchochea maendeleo ya kiuchumi kupitia rasilimali za maji, pamoja na kuongeza uwekezaji katika sekta hiyo.
Alitaja maeneo ya kipaumbele kuwa ni pamoja na utekelezaji wa Mpango Kabambe wa Kitaifa wa Maji, ujenzi wa Gridi ya Taifa ya Maji, uendelezaji wa mabwawa ya kimkakati, kuimarisha huduma za maji na usafi wa mazingira, pamoja na kujenga miundombinu inayohimili athari za mabadiliko ya tabianchi.
Aidha, alisisitiza umuhimu wa kuimarisha ushiriki wa sekta binafsi na kubuni njia mbadala za upatikanaji wa fedha ili kufanikisha utekelezaji wa miradi mikubwa ya maji.
Mkutano huo umehudhuriwa na viongozi wa Serikali, wadau wa maendeleo, sekta binafsi, asasi za kiraia na wataalamu wa sekta ya maji kutoka ndani na nje ya nchi.









No comments:
Post a Comment