GAVANA TUTUBA AWATOA HOFU WAWEKEZAJI SEKTA YA FEDHA NCHINI - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Tuesday, March 17, 2026

GAVANA TUTUBA AWATOA HOFU WAWEKEZAJI SEKTA YA FEDHA NCHINI


Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Bw. Emmanuel Tutuba, amewakaribisha na kuwatoa hofu wawekezaji wa kimataifa katika sekta ya fedha nchini Tanzania, huku akisisitiza kuwa mazingira ya uwekezaji ni rafiki.

Gavana Tutuba ameyasema hayo leo Jumanne Machi 17, 2026 katika mahojiano maalumu yaliyofanyika ofisini kwake makao makuu ya BoT jijini Dodoma.

“Kwa wawekezaji katika sekta ya fedha na sekta nyingine, huu ni wakati sahihi zaidi wa kuwekeza kwa sababu Tanzania ina soko kubwa, utulivu wa kisiasa na kiuchumi, pamoja na dira ya maendeleo ya taifa iliyo wazi pia tuna sera zinazounga mkono uwekezaji,” amesema Gavana Tutuba.

Akizungumzia usalama wa uwekezaji katika sekta ya fedha, Gavana Tutuba amesema BoT inaendelea kuisimamia kwa karibu sekta hiyo ili kuhakikisha inaendelea kuwa thabiti na salama kwa wawekezaji.

Amefafanua kuwa BoT inaendelea kuboresha mifumo ya usimamizi wa taasisi za fedha, ikiwemo kuanzisha mfumo wa kisasa wa usimamizi wa papo kwa papo (Real-Time Supervision System).

Kwa mujibu wa Gavana huyo, mfumo huo utawezesha ujumuishaji wa taarifa za kifedha kwa wakati halisi, hivyo kuifanya Benki Kuu kutambua mapema changamoto zinazoweza kujitokeza katika taasisi za fedha.

Aidha, Gavana Tutuba amebainisha kuwa pamoja na mazingira hayo bora ya uwekezaji, uchumi wa Tanzania unaendelea kukua kwa kasi ambapo kwa mwaka 2026 uchumi wa nchi unatarajiwa kukua kwa asilimia 6.3, kiwango ambacho ni kikubwa zaidi kuliko wastani wa ukuaji wa uchumi duniani, jambo linaloashiria fursa kubwa zaidi za uwekezaji katika sekta mbalimbali.

No comments:

Post a Comment