AWESO AAGIZA UDHIBITI WA UPOTEVU WA MAJI, ATAKA HATUA KALI DHIDI YA WAHUJUMU MIUNDOMBINU - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Wednesday, April 15, 2026

AWESO AAGIZA UDHIBITI WA UPOTEVU WA MAJI, ATAKA HATUA KALI DHIDI YA WAHUJUMU MIUNDOMBINU




Na Mwandishi Wetu, Dodoma


Waziri wa Maji, Mhe. Jumaa Aweso (Mb.) amewaagiza Viongozi wa Mikoa na Wilaya kupitia Kamati za Usalama kushiriki kikamilifu katika ulinzi wa miundombinu ya maji na kuhakikisha wanaojihusisha na uharibifu wanachukuliwa hatua kali, ikiwemo kushitakiwa kwa uhujumu uchumi.

Aidha, Waziri Aweso ameziagiza Mamlaka za Majisafi nchini kudhibiti upotevu wa maji katika maeneo yao, akisisitiza kuwa hilo ndilo kipimo kikuu cha utendaji kwa Wakurugenzi wa mamlaka hizo.

Akizungumza jijini Dodoma wakati wa uzinduzi wa Bodi mpya ya 10 ya Wakurugenzi ya Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dodoma (DUWASA), amesema tathmini ya Wizara imebaini kuwa baadhi ya maeneo yamefanikiwa kudhibiti upotevu wa maji huku mengine yakiendelea kukumbwa na changamoto hiyo.

“Niwaombe na niwasihi sana watendaji wa mamlaka zetu za maji, twendeni tukadhibiti upotevu wa maji; faraja ya Mkurugenzi ni kuona wananchi wanapata maji,” amesema Aweso.

Ameeleza kuwa upotevu wa maji ni miongoni mwa mambo yanayomkera kutokana na kusababisha hasara ya mapato, akisisitiza kuwa lengo kuu ni kuhakikisha wananchi wanapata huduma ya maji kwa uhakika.

Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji, Mhe. Rose Ambrose amesema uvujaji wa maji unasababisha hasara kubwa zisizo na msingi, huku baadhi ya hasara hizo zikichangiwa na uzembe wa watumishi.

Naye Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi DUWASA, Bw. Fadhili Chibago amesema bodi hiyo iko tayari kutekeleza maagizo yote yaliyotolewa na Waziri ili kuboresha huduma ya maji na mazingira katika Jiji la Dodoma.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa DUWASA, Mhandisi Aron Joseph amesema miradi ya kimkakati ikiwemo Bwawa la Farkwa na ule wa Ziwa Victoria inaendelea kutekelezwa ili kuboresha upatikanaji wa majisafi.

Ameongeza kuwa DUWASA itaendelea kubuni na kutekeleza miradi mingine kupitia wataalamu wa ndani ili kukabiliana na changamoto ya maji na kuboresha huduma kwa wananchi.












No comments:

Post a Comment