Na MWANDISHI WETU
SERIKALI imepokea rasmi hoja ya ajira za muda (part-time) kwa vijana iliyowasilishwa na Mbunge wa Kisarawe, Dk. Selemani Jafo, na kuanza mchakato wa kuichakata ili kubaini namna bora ya utekelezaji wake.
Akizungumza mara baada ya kupokea hoja hiyo kwa niaba ya Waziri Mkuu, Waziri wa Nchi, Sera, Bunge na Watu Wenye Ulemavu, Profesa Paramangamba Kabudi, amesema serikali inatambua uzito wa hoja hiyo na itaifanyia uchambuzi wa kina kabla ya kuchukua hatua stahiki.
Amesema hoja hiyo inalenga kutoa suluhisho la changamoto ya ajira kwa vijana, hivyo serikali itaipitia kwa makini ili kuona namna inavyoweza kutekelezwa kwa ufanisi na tija kwa taifa.
Aprili 9 mwaka huu, wakati akichangia hotuba ya Bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu, Dk. Jafo aliwasilisha hoja hiyo bungeni akipendekeza kuanzishwa kwa mpango maalumu wa ajira za muda mfupi kwa vijana nchini.
Katika hoja yake, Dk. Jafo alisema mpango huo utasaidia vijana kupata ajira za mikataba ya muda, kujenga uzoefu wa kazi na kupata kipato, sambamba na kuunga mkono juhudi za Rais Samia Suluhu Hassan za kuendelea kutoa ajira kwa vijana.
Alifafanua kuwa mpango huo unaweza kuanza kwa kuwahusisha vijana 50,000 wenye elimu ya stashahada na shahada, ambapo wa stashahada wangelipwa takribani Sh500,000 na wa shahada Sh700,000 kwa mikataba ya miaka mitatu.
Kwa mujibu wa maelezo yake, utekelezaji wa mpango huo unaweza kugharimu takribani Sh bilioni 396, huku ukilenga kupunguza tatizo la ajira na kuwajengea vijana uzoefu wa vitendo.
Aidha, alieleza kuwa hali ya sasa inaonesha vijana wengi wahitimu wanajikuta wakifanya kazi zisizoendana na taaluma zao, ikiwemo bodaboda, jambo alilosisitiza linahitaji hatua za haraka za kisera.
Pia alipendekeza utekelezaji wa mpango huo uanze kwa makundi maalumu yakiwemo walimu, wahudumu wa afya na vijana waliopo mitaani, huku ukiratibiwa kupitia mamlaka za serikali za mitaa ili kuongeza ufanisi.

No comments:
Post a Comment