Tanzania imeendelea kufungua milango ya uwekezaji kwa kuonesha fursa mbalimbali zilizopo, hususan katika sekta ya viwanda, kwa lengo la kuongeza uzalishaji na ajira nchini. Hatua inayolenga kuvutia wawekezaji wa kimataifa na kuimarisha uchumi wa taifa.
Katika kuendeleza juhudi hizo, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Uwekezaji na Maeneo Maalum ya Kiuchumi (Tanzania Investment and Special Economic Zones Authority- TISEZA), Bw. Gilead Teri, amewahimiza wawekezaji kutoka Belarus kuchangamkia fursa zilizopo nchini.
Ameyasema hayo alipokutana na Waziri wa Mambo ya Nje wa Belarus, Mhe. Maxim Ryzhenkov, aliyefanya ziara katika Eneo Maalum la Kiuchumi la Benjamin Mkapa linalosimamiwa na TISEZA, tarehe 29 Aprili 2026, jijini Dar es Salaam.
Bw. Teri ameeleza kuwa Tanzania, kupitia TISEZA, imejipanga kikamilifu kuwezesha biashara na uwekezaji kwa kuboresha mazingira ya uwekezaji pamoja na kurahisisha taratibu kwa wawekezaji wa ndani na nje ya nchi. Akisisitiza uwepo wa fursa nyingi katika sekta ya viwanda, ikiwemo upatikanaji wa ardhi ya viwanda.
Kwa upande wake, Mhe. Ryzhenkov ameeleza kuvutiwa na mazingira ya uwekezaji nchini na kuipongeza Serikali kwa juhudi zake za kuboresha miundombinu na mifumo ya biashara. Akisisitiza kuwa Belarus iko tayari kuimarisha ushirikiano na Tanzania katika sekta za viwanda, biashara na uwekezaji kwa manufaa ya pande zote mbili.
Katika ziara hiyo, Mhe. Ryzhenkov alitembelea kiwanda cha kushona nguo za jeans cha Tooku na kujionea mchakato wa uzalishaji wa nguo kwa ajili ya soko la nje, akiambatana na Balozi wa Tanzania nchini Urusi, Mhe. Fredrick Kibuta, pamoja na Balozi wa Belarus nchini, Mhe. Dzmitry Krasouski.








No comments:
Post a Comment