Na Mwandishi Wetu, OKULY BLOG, DODOMA
Waziri wa Katiba na Sheria, Dkt. Juma Zuberi Homera, amewataka watumishi wa umma kutumia kwa uangalifu magari ya serikali, akisisitiza kuwa ni mali ya walipa kodi inayopaswa kutunzwa ili kudumu na kutoa huduma iliyokusudiwa.
Akizungumza Aprili 15, 2026 jijini Dodoma wakati wa hafla ya kukabidhi vitendea kazi kwa Mahakama ya Tanzania na Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, Dkt. Homera amesema matumizi mabaya ya magari yanaweza kuisababishia serikali hasara na kudhoofisha utoaji wa huduma kwa wananchi.
“Magari haya yatunzwe na yatumike kwa uangalifu. Ni mali ya serikali inayotokana na fedha za walipa kodi, hivyo ni wajibu wetu kuyahifadhi,” amesema.
Ameeleza kuwa wizara imeendelea kuziimarisha taasisi hizo kwa kuzipatia magari ya kisasa na vifaa muhimu, ikiwemo kompyuta 150 kwa Mahakama ya Tanzania, na magari 5 na kompyuta 30 kwa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, hatua itakayoboresha utoaji wa huduma za haki.
Aidha, amewapongeza watumishi wa mahakama kwa juhudi zao katika kusimamia haki kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977.
Kwa upande wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, amesema ina jukumu muhimu la kulinda haki za binadamu na kupokea malalamiko ya wananchi, huku akibainisha kuwa serikali inaendelea kukabiliana na changamoto za upungufu wa vitendea kazi ili kuongeza ufanisi.
Dkt. Homera pia ameishukuru Shirika la Mpango wa Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) kwa ushirikiano wake katika kuboresha sekta ya sheria nchini, akisema ushirikiano huo utaendelea kuimarishwa.
Amesisitiza kuwa serikali inalenga kutumia TEHAMA kuunganisha mifumo ya taasisi za umma ili kuongeza ufanisi na kuwafikia wananchi wote kwa urahisi, ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050.








No comments:
Post a Comment